Na Asha Mwakyonde, Dodoma
UTAFITI wa Athari za Upatikanaji wa Nishati Endelevu Tanzania Bara kwa mwaka 2021/2022, unaonesha asilimia 72 ya Kaya zote zimefikiwa na umeme huku usambazaji umeme huo vijijini wafikia asilimia 90.
Pia Utafiti huo umefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351 Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ukiwa lengo la kuiwezesha Serikali kutathmini na kufuatilia programu mbalimbali za maendeleo, kutunga sera, na pia kufanya maamuzi sahihi ya mipango ya maendeleo kwa kutumia ushahidi wa takwimu.
Akizungumza jijini Dodoma leo Novemba 10,2023 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko wakati akizindua utafiti huo alisema Serikali imetimiza lengo namba 7 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG 7) linaloelekeza kwamba ifikapo mwaka 2030 kuwe na uhakika wa upatikanaji wa huduma za nishati nafuu, za kuaminika, na za kisasa kwa wote.
"Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kupima upatikanaji wa nishati endelevu na athari ya upatikanaji wake kwa Tanzania Bara," alieleza Dk. Biteko.
KUHUSU REA
Akizungumzia WAKALA ya Nishati Vijijini (REA), DK.Biteko alisema
taarifa ya Wakala huo ya mwezi Novemba 2023, inaonesha jumla ya vijiji vilivyounganishwa na umeme Tanzania Bara ni 11,079 sawa na asilimia 90 ya vijiji vyote 12,318, na vilivyobaki ni 1,239 sawa na asilimia 10 ambapo vinatarajiwa kuunganishwa na umeme ifikapo Juni 2024.
"Serikali imeanza kupeleka umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara na upelekaji wa umeme huu umeanza mwaka 2023/24 kwa kupeleka umeme katika vitongoji 15 katika kila jimbo," amebainisha
Alifafanua kuwa Serikali kupitia REA inatekeleza mradi wa kusambaza mifumo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua katika makazi kwenye visiwa 41 vya Mikoa ya Kagera, Lindi, Mara, Mwanza na Rukwa. Serikali pia kupitia REA inatoa uwezeshaji wa kiufundi na kifedha kwa waendelezaji wa miradi midogo ya nishati jadidifu katika maeneo ya vijijini ili kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini.
NISHATI YA KUPIKIA
Dk. Biteko alisema Serikali inakamilisha Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia
unaojikita katika kutatua vikwazo vinavyokwamisha matumizi ya nishati hiyo huku lengo likiwa ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaitumia ifikapo mwaka 2033
"Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuhamasisha matumizi ya LPG kwa kuwapatia wananchi mitungi ya gesi na vifaa vyake ambapo katika mwaka 2023/24 kupitia REA tumepanga kutoa mitungi 200,000 ya LPG na vifaa vyake kwa wananchi pamoja na mifumo ya kupikia ya gesi asilia katika taasisi mbalimbali za umma.
Aidha, Dk. Biteko alisema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya Upatikanaji wa nishati endelevu ambapo amewahakikishia wananchi kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi na za muda wa kati zitakazowezesha kufikia lengo la nishati safi kwa haraka zaidi.DK.Biteko.
Awali Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba alisema kuwa matokeoa hayo ya
asilimia 72 ya Kaya zote kufikiwa na umeme ni mafanikio makubwa kwa nchi na kwamba yameshinda nchi nyingne za Ulaya.
" Nikuhakikishie Wizara ya fedha itayasambaza matokeo haya ya Utafiti huu ili yaweze kutumika," asema Waziri Nchemba.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa utafiti huo ni kati ya tafiti ambazo zilishafanyika.
"Utafiti huu umefanyika katika mikoa yote Tanzania Bara na mafanikio ni makubwa katika upatikanaji wa nishati,"alisema Mtakwimu huyo.
Utafiti huo umefanywa kwa kushirikiana na Ofisi ya Takwimu ya Norway (SSB), pamoja na wadau muhimu wa nishati ambao ni Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ulifanyika katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
0 Comments