WAZIRI MKUU MGENI RASMI MAADHIMISHO YA UKIMWI


Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni katika  Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo yatafanyika Kitaifa mkoani Morogoro  Disemba mosi mwaka huu na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania 
(TACAIDS).

Wananchi na wadau wote kushirikiana katika kupanga na kutekeleza shughuli za kudhibiti VVU na UKIMWI kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya mahali walipo lengo likiwa ni kuhakikisha Usawa hasa wa kijinsia na utoaji huduma ni nguzo kubwa ya  kutimiza ndoto ya serikali  kumaliza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Haya yamesemwa leo Oktoba 14,2023 jijini  Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu  Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho hayo alisema maeneo yanayohitaji msukumo na vipaumbele ni pamoja na kuimarisha afua za VVU na UKIMWI kwa vijana kwani takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, kundi la
vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 linachangia maambukizi
mapya ya VVU kwa asilimia 40 na hivyo kulifanya kundi hilo kuwa
kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya VVU. 

Waziri Mhagama amesema, huduma za VVU na UKIMWI zinaendelea kutolewa kwa kiwango cha kuridhisha,Upimaji wa hiari na utoaji wa dawa za ARV umekuwa na mafanikio makubwa kwa kuzingatia kigezo cha malengo ya 95 - 95 – 95. 

Waziri Mhagama amefafanua kuwa hiyo ina maana asilimia 95 ya watu walio na maambukizi ya VVU
wawe wametambua hali zao, Asilimia 95 ya wale wanaotambua
kuwa wanaishi na VVU wawe wanatumia dawa za ARV na
asilimia 95 ya wale wanaotumia ARV wawe wamefubaza VVU
mwilini.

Amebainisha kuwa kipimo cha utendaji wetu katika kufikia malengo hayo watakipata Desemba 1, 2023 baada ya kutangazwa na
mgeni Rasmi kufuatia kukamilika kwa Utafiti wa Viashiria vya
VVU na UKIMWI (Tanzania AIDS Impact Survey - THIS) wa mwaka 2022/23 ambao utatoa picha ya hali halisi ilivyo sasa.


Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini uongozi wa Jemadari Rais 
Dk. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwekeza kwenye afya yajamii kupitia ujenzi wa miundombinu ya hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati kote nchini.

 "Kwa kawaida siku hii huadhimishwa ndani ya wiki moja ambapo shughuli mbalimbali zinazohusu Utoaji wa taarifa za udhibiti wa VVU na UKIMWI na huduma ya Upimaji wa hiari wa VVU zitafanyika kuanzia Novemba 24, 2023 hadi siku ya kilele ya Desemba mosi, mwaka huku," amesema Mhagama. 

Waziri huyo ameongeza kuwa huduma mbalimbali zikiwemo upimaji,ushauri na shughuli zote zinazotekelezwa na wadau wa UKIMWI zitatolewa kwenye mabanda ya maonesho yatakafanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Ameeleza kuwa kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo katika mwaka 2023 ambayo ni fursa nzuri ya kuelezea mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kusukuma mbele ajenda ya kutokomeza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ni “Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI”(Let Communities Lead).

 "Kauli mbiu hii inaangazia umuhimu wa kutoa nafasi kwa jamii kushika hatamu kuelekea kutokomeza
UKIMWI," alisema Waziri Mhagama na kuongeza.

Katika Maadhimisho hayo, kutakuwa na wageni waalikwa kutoka katika maeneo mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Mabalozi,
wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Wadau wa
Maendeleo, Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Madiwani,
Viongozi wa Dini, Asasi za Kiraia pamoja na wananchi kwa ujumla," amesema.

"Nitumie fursa hii kuagiza Kamati za UKIMWI za ngazi zote
katika Halmashauri zetu, Wizara na Idara zote za Serikali, Asasi
za Kiraia, Taasisi za Dini za madhehebu yote na vyombo vya
habari kutumia siku hii kutafakari kwa kina michango na nafasi
yao katika kutokomeza UKIMWI nchini," ameeleza.

Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inaratibu maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo yaliasisiwa na Shirika la 
Afya Duniani (WHO) Mwaka 1988 na kisha kuanza kuratibiwa na 
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Udhibiti wa 
UKIMWI Duniani (UNAIDS).

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI