NSOKOLO: WAANDISHI WA HABARI WALINDWE DHIDI YA UHALIFU

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

RAIS wa Muungano wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) ,Deogratius Nsokolo ametoa wito kwa vyombo vya Dola nchini kuwalinda Wandishi wa Habari dhidi ya uhalifu pindi unapotokea wakiwa katika majukumu yao ya kazi.

Nsokolo ametoa Wito huo leo Novemba 2,2023 wakati akifungua mdahalo ulioandaliwa na UTPC  kupitia mkutano wa 'Zoom' ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya kukomesha Uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari  (International Day to End Impunity for Crimes against Jornalist). 

Nsokolo amesema wakati wanaadhimisha siku hiyo, UTPC, Serikali na wadau wengine waendelee kuhakikisha kwamba uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine, Vyombo vya Dola vyenye jukumu la kulinda usalama wa Raia na mali zao, vichunguze matukio ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari.

Ameongeza kuwa UTPC inaweza kutoa jukwaa la msaada wa Ulinzi kwa waandishi wa habari wanaokumbana na vitisho au uhalifu katika kutekeleza majukumu yao ambapo ushirikiano kati ya waandishi wa habari na UTPC unaweza kuimarisha usalama wao na kuwawezesha kufanya kazi zao kwa uhuru.

“Lakini pi tuendelee kutumia Klabu zetu kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa Uhuru wa vyombo vya habari na jukumu la waandishi wa Habari katika jamii. Hii inaweza kusaidia kupunguza hali ya uhasama dhidi ya Waandishi wa Habari,”ameeleza Nsokolo. 

Aidha ameeleza kuwa Umma ukielimishwa unawezaa kushiriki zaidi katika mchakato wa kisiasa na kijamii na hivyo kuwa na mchango mzuri sana katika ujenzi wa Taifa. Kwa kuelewa jukumu la waandishi wa habari katika masuala ya umma, umma unaaweza kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao

Novemba 2, kila mwaka kuanzia mwaka 2013, Duniani kote huaadhimishwa Siku ya Kimataifa ya kukomesha Uhalifu Dhidi ya Waandishi wa Habari, (International Day to End Impunity for Crimes against Journalists).

Kwa mwaka 2023, Maadhimisho haya yanalenga kuongeza uelewa kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao, lakini pia kuonya juu ya kukithiri kwa vitendo vya ukatili na ukandamizaji dhidi ya waandishi wa Habari

Mdahalo huu umeshirikisha waandishi wa habari kutoka Klabu zote Tanzania Bara na visiwani, Sekretarieti ya UTPC, Wajumbe wa Bodi ya UTPC, Waratibu kutoka Klabu za Waandishi wa Habari pamoja na wadau wengine wa habari na wahisani.


Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI