Na Asha Mwakyonde,Dodoma
SERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),imesema kuwa zaidi ya Megawati 197 zimeongezeka katika mfumo wa Gridi ya Taifa ndani ya kipindi cha kati ya mwezi Septemba mwishoni hadi kufikia sasa kutokana na juhudi mbalimbali za matengenezo ya mitambo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa Gesi Asilia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Pia hali ya uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo vya maji bado haijaimarika kutokana na mvua kuchelewa kuanza kunyesha katika mikoa ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji kwenye vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia maji vya Mtera, Kidatu na Kihansi na mikoa ya Iringa, Mbeya, Tabora, Singida na Dodoma.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma leo Novemba 24,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Gissima Nyamo- Hanga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya upatikanaji wa umeme nchini amesema kuwa ongezeko hilo ni kutokana na mvua zinazonyesha katika ukanda wa vituo vya kuzalisha umeme vya Nyumba ya Mungu, Hale na Pangani.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa katika kipindi tajwa upungufu wa upatikanaji wa umeme umeweza kushuka kutoka Megawati 410 hadi kufikia Megawati 213 kwa sasa.
Amesema mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya ukanda wa Pwani hususani katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga na zile zinazoendelea kunyesha katika Ukanda ya Ziwa Victoria katika Mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera ni mvua ambazo kwa ujumla mtiririko wake wa maji hauelekei viliko vyanzo vyetu vya kuzalishia umeme vya Mtera, Kidatu na Kihansi.
Mhandisi huyo ameongeza kuwa hali ya upatikanaji wa umeme itaendelea kuimarika katika miezi ya usoni kutokana na kukamilisha matengenezo ya mitambo iliyokuwa na hitilafu, kuongezeka kwa uzalishaji wa Gesi asilia, kukamilika kwa mradi wa Rusumo utakaotupatia Megawati 27 na Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2115.
"Kwa sasa kumeanza kuwepo kwa dalili ya mvua katika Mikoa hiyo jambo linaloashiria kuwepo kwa uongezekaji wa uzalishaji wa umeme katika vituo hivyo kwa kipindi cha muda mfupi kutoka sasa," amesema Nyamo-Hanga.
Akizungumzia utelekezaji wa mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere Mhandisi Nyamo-Hanga ameeleza kuwa umefikia zaidi asilimia 94.
"Shirika linawashukuru wateja wake wote na wadau mbalimbali wa sekta ya umeme na kuwaomba kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito, na kwamba Shirika litaendelea kutoa taarifa za hali ya upatikanaji wa umeme kwa kadri hali itavyozidi kuimarika," amesema.
Mhandisi Nyamo-Hanga amesema ili kuhakikisha ubora wa huduma kwa wateja unaongezeka, Shirika litaimarisha ukubwa wa kituo chake cha mawasiliano kwa wateja kwa kuongeza idadi ya watoa huduma wanaopokea na kujibu simu za wateja kutoka 65 hadi kufikia 100 ili kumudu ongezeko la simu za wateja ifikapo katikati ya mwezi Januari mwaka 2024.
0 Comments