ZALISHENI WATAALAM WENYE USHINDANI KATIKA SOKO LA AJIRA- RAIS DKT. SAMIA

Na WMJJWM, Arusha

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa vyuo na taasisi kuzalisha wataalam wanaoweza kujiajiri na wanaokubalika katika soko la ajira. Aidha, amezitaka taasisi na vyuo kuwekeza katika tafiti za maendeleo zenye kuchangia kuleta suluhisho ya changamoto kwenye jamii na Taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa kwa niaba yake na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua Kongamano la Wataalam wa Maendeleo ya Jamii na Maadhimisho ya Miaka 60 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Novemba 20, 2023 jijini Arusha.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Rais Samia anatambua mchango mkubwa wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na wataalam wa maendeleo ya jamii nchini na ana matarajio makubwa zaidi baada ya miaka 60. 

Amewaasa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kutumia taaaluma yao na mbinu shirikishi katika kuwezesha jamii kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili hivyo Vyuo na Taasisi za mafunzo ya wataalam wa maendeleo ya jamii waendelee kuzalisha wataalam mahiri wanaoendana na soko la ajira na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ikiwepo ufuatiliaji wa wahitimu.

Aidha, Waziri Dkt. Gwajima ameelekeza uongozi wa Chama cha Wataaluma wa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA) kuhakikisha wanakamilisha mchakato wa kuunda Sheria ya Taaluma ya Maendeleo ya Jamii itakayosimamia utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kusimamia miiko, maadili ya taaluma hiyo kwa masilahi mapana ya taifa.

"Wataalam wa Maendeleo ya Jamii katika sekta mbalimbali nchini ni chachu katika kuleta maendeleo ya jamii na nchi. Ni matarajio yangu kuwa mkitekeleza majukumu yenu ipasavyo tutakuwa na jamii yenye fikra na mtazamo chanya katika maendeleo, yenye maadili mema, malezi na makuzi chanya ya watoto, jamii isiyo na ukatili wa kijinsia, yenye uzalendo kwa nchi yao, inayofanya kazi kwa bidii na kujitolea, jamii inayojali na kuhifadhi rasilimali za nchi; yenye lishe na afya bora, yenye matumizi sahihi ya TEHAMA na inayojiwekea akiba," amesema Waziri Dkt. Gwajima. 

Naye Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda pamoja na Waziri Mstaafu wa Maendeleo ya Jamii Dkt. Anna Abdallah wakizungumza katika Kongamano hilo, wamesema kada ya Maendeleo ya Jamii ni kitovu cha maendeleo kuanzia ngazi ya kitongoji na wameshauri Serikali kuipa kipaumbele kwa kuiimarisha zaidi ili kufanya kazi yake kwa ufanisi na kusaidia wananchi kuhamasika katika shughuli zote za maendeleo.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Steven Mutambi amesema Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ni muhimu nchini kwani wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kufanikisha masuala mbalimbali kuanzia ngazi ya vijiji hasa katika uhamasishaji wa wananchi kushiriki shughuli za Maendeleo. 

Kongamano hilo la 16 la Wataalam wa Maendeleo ya Jamii linafanyika kwa siku 3 likiambatana na Maadhimisho ya miaka 60 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, ambapo kaulimbiu ya kongamano la mwaka 2023 ni "Sekta ya Maendeleo ya Jamii: Msingi Imara wa Uwezeshaji wa Wananchi."

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI