SERIKALI YATOA MISAADA YA KIBINADAMU KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO KILIMANJARO

Naibu Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.  Ummy Nderiananga akikabidhi misaada ya kibinadamu kwa baadhi ya waathirika wa mafuriko wakati  alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maeneo yaliyoathirika katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Naibu  Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akitembelea na kukagua baadhi ya nyumba ziliozoathirika na mafuriko  wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Amir Mkalipa akitoa taarifa ya Maafa katika Wilaya hiyo wakati ziara ya Naibu  Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga alipowasili katika Wilaya hiyo  kukabidhi misaada ya kibinadamu kwa baadhi ya waathirika wa  mafuriko  mkoani Kilimanjaro.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi akifafanua jambo katika ziara ya Naibu  Waziri  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga alipowasili katika Wilaya hiyo  kukabidhi misaada ya kibinadamu kwa baadhi ya waathirika wa  mafuriko  mkoani Kilimanjaro.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro

SERIKALI imetoa misaada ya vyakula, magodoro, ndoo, madumu na mablanketi kwa kaya 119 za Kata Nane za Halmashauri ya Wilaya  ya  Moshi mkoani Kilimanjaro zilizokumbwa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. 

Akikabidhi misaada hiyo amabyo ni mahindi tani 20, magodoro 150, mablanketi 300, ndoo 150, madumu 150, na mikeka 300  Naibu  Waziri Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe.  Ummy Nderiananga amesema kuwa, Serikali inatambua changamoto iliyowakumba wananchi hao kutokana na mvua zilizonyesha na kusababisha  mafuriko.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ametumia nafasi hiyo  kutoa onyo kwa baadhi ya watu wanaotoa taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii kucha mara moja tabia hiyo kwani wanasababisha taharuki.

"Inapotokea taarifa za maafa wapo wasemaji wake kwa mkoa ni Mkuu wa mkoa na wilaya ni Mkuu wa wilaya sasa wapo watu wanarekodi na kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao na kusababisha taharuki kubwa niwaombe achaneni na hii tabia tumieni mitandao vizuri," alisema Naibu Waziri Ummy. 

Vile vile  Naibu Waziri huyo  ameiagiza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi kukutana na kamati ya maafa ya Wilaya pamoja na wataalam wengine ili kuweka mikakati ya uzibuaji wa njia za mto Nanga na mto Manguvu ili kuzuia mafuriko katika Kijiji cha Saningo, Kata ya Old Moshi. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Mhe. Prof. Patrick Ndakidemi alitumia nafasi hiyo kuishikuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo wamezikimbilia familia za waathirika  wa mafuriko katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Hanang mkoani Manyara. 

Prof. Ndakidemi alisema kuwa, katika maafa hayo yaliyosababishwa na mvua jumla ya watu watano walifariki dunia pamoja na mashamba na vitu mbalimbali vikiwemo vyakula kusombwa na mafuriko. 

"Msaada uliotolewa na serikali utasaidia kuzifariji familia ambazo zimekumbwa na mafuriko pamoja na kuwafariji watu ambao ni waathirika  hatua hii ni kuonyesha jinsi ambavyo Serikali inawathamini" alisema Prof. Ndakidemi. 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe. Amir Mkalipa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi aliutaka  uongozi  wa Halmashauri kuhakikisha wanagawa vitu hivyo kulingana na maelekezo ya serikali na yeyote atakayekiuka hatosita kumchukulia hatua. 

Kwa upande wao waathirika waliishukuru Serikali  kuwajali wananchi wake wakati wote wanapokumbwa na changamoto  hatua ambayo huwapa faraja na kusaidia kurejesha hali.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI