Na Asha Mwakyonde Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imesema kuwa katika ripoti ya gesi asilia wanawahamasisha watu wenye magari warekebishe magari yao ili watumie gesi asilia iliyokandanizwa (CNG).
Haya yamesemwa jijini Dar es Salaam leo Julai 5, 2024 na Meneja Mawasiliano na Uhusiano EWURA Titus Kaguo katika maonesho ya 48 ya kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), kwenye banda la mamlaka hiyo,amesema katika banda hilo kuna ripoti mbalimbali za utendaji wa sekta ya umeme, maji, petroli na ile ya gesi asilia.
"Wale wanaotaka kuwekeza tutawaambia wawekeze katika vituo vya gesi asilia iliyokandamizwa Kwani Tanzania inawezekana," ameeleza.
Amesema Shirika la Viwango Tanzania (TBS), tayari lilishafanya marekebisho ya viwango vya ubora ambapo kituo chochote cha mafuta Tanzania kinaweza kujumuisha kituo cha gesi asilia (CNG).
Amefafanua kuwa ili CNG iweze kutumika nchi nzima itaenda kwa awamu tofauti na bidhaa nyingine na kwamba hilo ni kwa mujibu WA maelekezo ya wizara kwamba EWURA ichukue kama chanzo kingine cha matumizi ya nishati mbadala kutokana na hali mafuta duniani.
Aidha ameishukuru Wizara ya Nishati kwa utendaji bora pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, kwa muogonzo ambao wanatupatia ili waweze kufanya kazi vizuri huku akimshuru Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk.James Andilile.
Kaguo amesema kuwa katika banda hilo wataalam wote wapo wa gesi asilia, sekta ya maji, petroli, huku akisema wamejipanga kutoa elimu na kuhakikisha kila changamoto inatatuliwa.
" Tumekuja hapa kwa maelekezo maalum kama tunavyojua Wizara ya Nishati imejipanga kutoa taarifa kwa Umma, taarifa hizi ni nyenzo kwa shughuli ambazo tunazifanya kama tunavyoagizwa kiongozi wetu, Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko ambaye ni Waziri wa Nishati anataka taarifa zitolewe kwa Umma," amesema.
Ameeleza kuwa hata alivyokuwa akizindua ripoti za taarifa za utendaji wa nishati moja ya maelekezo yake anataka taasisi zitoe taarifa kwa Umma ili watanzania wajue wizara inachokifanya.
" Kuna kina mama wamefika hapa wanataka kuungiwa gesi na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), tumewaelekeza kinachotakiwa, lakini tumewaelekeza waende TPDC ili waweze kuelewana na kuungiwa gesi na hii inakuwa ni majibu ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye anataka Tanzania iwe ni moja ya nchi bora kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ameongeza wapo katika maonesho hayo kutoa taarifa kwa Umma juu ya majukumu ambayo wanayafanya yakiwamo ya kudhibiti Petroli na bidhaa zake, umeme na gesi asilia, maji na usafi wa mazingira.
Ameelezea kuwa watanzania wengi wamekuwa wakipatiwa elimu ya kutosha huku akisema watu waliofika katika banda hilo ni wale wenye shauku ya kuwa na leseni ya umeme.
Amesema wizara iliipatia EWURA mamalaka ya kutoa leseni ndogo za ukandarasi zenye madaraja mbalimbali huku akieleza kwamba utaratibu ea kupata leseni hizo zipo kwenye mtandao.
0 Comments