Na Asha Mwakyonde Dar es Salaam
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limesema kuwa limejipanga kufungua milango ya kidigitali kwa wawekezaji ili waweze kufanya biashara kwa usahihi zaidi bila kukumbana na changamoto kwenye masuala ya mtandao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 3,2024 jijini Dar es Salaam katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TTCL, Zuhura Muro ameeleza kuwa Shirika hilo lipo tayari kufanya ushirikiano na wawekezaji nchini kwa lengo la kuhakikisha wanapata huduma nzuri ya Mawasiliano.
Muro amesema shirika hilo lina wajibu mkubwa wa kuunganisha Mawasiliano mahali popote ili kurahisisha biashara kufanyika kwa usahihi huku akisema hadi sasa jumla ya watalii 9000 wamejiunga na WiFi katika mlima Kilimanjaro hivyo wamejipanga vizuri kufungua milango ya digitali kuendesha biashara.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi amesema TTCL imekuwa ikiendesha mkongo wa Taifa hivyo wamejipanga kuhakikisha wanaendesha biashara kila sehemu.
Amesema kupitia ushirikiano waliokuwa nao utawawezesha wawekezaji kufanya shughuli zao mbalimbali bila kupata changamoto zozote na kurahisisha biashara kufanyika vizuri.
Aidha amesema wanatarajia kuwa kitovu cha malipo jamii na katika kusapoti utalii wanatarajia kupeleka Mawasiliano katika mlima Kilimanjaro.
0 Comments