Na Asha Mwakyonde,DODOMA
BODI ya Kahawa Tanzania (TCB), imesema kuwa ina mkakati wa kuongeza unywaji wa kahawa kutoka asilimia 7 hadi 8 ambao ni unywaji wa sasa kwenda ailimia 15.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Agosti 01, mwaka huu amezindua mradi wa mghahawa unaotembea maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu ili kuweza kutoa huduma ya unywaji wa kahawa.
Akizungumza leo Agosti 2, 2024 na waandishi wa habari kwenye maonesho ya wakulima na wafugaji nane nane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Primus Kimaryo amesema wamebuni mradi huo wa mghahawa unaotembea ili kuwaweza vijana kujipatia kipato kupitia zao hilo la kahawa.
Kimaryo amefafanua kuwa mradi huo unawalenga kuwakopesha vijana kwa gharama nafuu ambapo katika kipindi cha muda wa miaka mitatu anapaswa kumaliza kulipa mkopo huo na kwamba utakuwa ni mali yake.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa wanaanza kwa kutengeneza mighahawa 100 ya awali ambapo itatengenezwa kwa awamu.
"Vijana wameshaonesha nia ya kutaka kuwa na mgahawa huo na kujikwamua kiuchumi," ameeleza Mkurugenzi huyo wa TCB.
Ameongeza kuwa msukumo mkubwa ni kuona namna gani vijana wanaweza kuoata ajira kupitia zao la kahawa kwani kijana kupata ardhi au kukodisha mgahawa ni changamoto.
Kimaryo amesema kabla kupata mradi huo vijana wote wataokidhi vigezo watapatiwa mafunzo ya uendeshaji wa mighahawa hiyo ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa.
0 Comments