WANYAMAPORI WANA MCHANGO MKUBWA KATIKA SEKTA YA UTALII

Na Beatus Maganja 

AFISA Mhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Winniefrida Kweka amesema Wanyamapori waliopo nchini wana mchango mkubwa katika Sekta ya Utali kwakuwa huchangia zaidi asilimia 17 katika pato la Taifa.

Winniefrida ametoa kauli hiyo Agosti 04, 2024 alipokuwa akitoa elimu ya uhifadhi kwa mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma waliotembelea bustani ya wanyamapori hai iliyopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye maonesho ya NaneNane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni Mkoani humo.

"Wanyamapori wanachangia sana kwenye Sekta ya utalii kwa zaidi ya asilimia 17 za pato la nchi, asilimia zote hizi zinachangiwa na utalii unaohusisha wanyama wa porini" amesema.

Winniefrida amesema kutokana na faida zitokanazo na wanyamapori hao kwa nchi, TAWA inatumia maonesho hayo kuwaelimisha watanzania wote kuachana na mitazamo hasi kuwa wanyamapori ni viumbe wasio na mchango chanya kwa Taifa.

Aidha Mhifadhi huyo amesema kutokana na changamoto inayoletwa na baadhi ya wanyamapori wakali na waharibifu kama vile mamba, tembo, fisi na wengine, TAWA imekuwa ikielimisha umma juu ya mbinu rafiki za kuweza kuishi na wanyamapori hao na kuendelea kubaki salama kwa kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.

Vilevile Winniefrida amebainisha kuwa chanzo kikubwa cha migongano baina ya wanyamapori hususani mamba na binadamu ni pale ambapo binadamu anapokuwa anahitaji mahitaji yake sehemu ambapo wanyamapori hao wapo (majini).

Amesema kufuatia changamoto hiyo Serikali kupitia Taasisi zake za kiuhifadhi imekuwa ikitoa elimu ya kujilinda dhidi ya athari zinazoweza kusababisha na wanyama hao ikiwa ni pamoja na kusaidia katika ujenzi wa vizimba vya mfano ili kuepusha madhara ya wanyamapori hao.

Winniefrida ametoa wito kwa wavuvi kufanya shughuli zao za uvuvi kwa njia zilizo sahihi na kuepuka kutega mitego yao ya Samaki sehemu ambazo mamba walipo na kuachana na dhana iliyojengeka miongoni mwao kuwa palipo na mamba ndipo pana samaki wengi.

Maonesho ya mwaka huu yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Chagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, mifugo na uvuvi" yalianza tarehe Agosti 01, 2024 na yanategemewa kufika kilele Agosti 08, 2024.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU