WATU 1000 KUSHIRIKI JUKWAA LA UNUNUZI WA UMMA AFRIKA MASHARIKI

Na Mwandishi wetu Dodoma 

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Dennis Simba ameeleza kuwa, Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki linalotarajia kufanyika kuanzia Septemba 09-12 mwaka huu jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 8,2024 kwenye kilele cha maonesho ya nane nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni Jijini Dodoma Simba amesema, mgeni rasmi katika ufunguzi huo anatarajiwa kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye pia atazindua mfumo wa Ununuzi wa Umma wa Kielektroniki (NeST).

Hii ni mara ya nne kwa Tanzania kupata nafasi ya kuratibu na kuandaa jukwaa hilo ambalo linatoa fursa kwa wadau mbalimbali wa ununuzi ndani na nje ya nchi kwa sekta za umma na binafsi .

Amesema jukwaa hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 1000 kutoka nchi za Tanzania ,Kenya,Uganda,Burundi,Rwanda,Sudani Kusini,Somalia na Demokrasia ya watu wa Congo kutoka sekta ya Umma,sekta binafsi ,Mashirika ya kitaaluma,Asasi za Kiraia na Taasisi za mafunzo.

Simba amesema jukwaa hilo litatoa fursa ya kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika masuala ya ununuzi wa umma kwa nchi za Afrika Mashariki, ili kuleta maendeleo endelevu ya sekta ya ununuzi na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.

"Hili ni tukio ambalo linawakutanisha pamoja na kuleta muingiliano kwa wadau mbalimbali wa ununuzi wa umma na kutoa fursa kwa wadau na kuwasilisha kero zao na juhudi zao katika kuboresha na kujenga mazingira rafiki ya ununuzi wa umma katika ukanda wa Afrika Mashariki."amesema Simba

Akieleza faida za jukwaa hilo hapa nchini amesema ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na ubadilishanaji wa maarifa kati ya vyombo vya udhibiti wa ununuzi kutoka nchi wanachama wa Afrika ,kuimarisha uwazi,uwajibikaji katika utendaji kazi wa Serikali kwa kuboresha mifumo ya kitaasisi.

Vile vile amesema, jukwaa hilo linaipa PPRA na wadau wengine fursa ya kupata ujuzi na upashaji habari ambao ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza uwazi,kujenga uelewa wa ununuzi kwa wadau,kuwapa maarifa na ujuzi wadau wa kongamano hilo.

Mkurugenzi huyo ametumia nafasi hiyo kuwaalika wadau wote kushiriki katika kongamano hilo kwa ajili ya kupata uelewa na mambo mengi yanayohusu masuala ya ununuzi.

Aidha amesema, kongamano hilo litafungwa Sept 12 mwaka huu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

#NTTupdates

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU