WATU 387 WAMEPATIWA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA KWENYE MAONESHO YA NANE NANE DODOMA

 
Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

KATIBU Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi, amesema kuwa idadi ya watu waliofika katika banda la Wizara hiyo kupata msaada wa kisheria kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane),ambayo yanafanyika Kitaifa viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma hadi kufikia jana imefika 387 kati yao 195 ni akina mama na akina baba ni 192 ni wanaume.

Akizungumza leo Agosti 6,2024 katika maonesho hayo kwenye banda la Wizara hiyo Maswi amefafanua kuwa kati ya akina mama hao 195 waliofika katika banda hilo wengi wao walihitaji msaada wa kisheria kwenye maeneo ya Ardhi na mirathi.

Ameeleza kuwa wengi waliojitokeza kutaka msaada huo wa kisheria ni katika eneo la Ardhi huku akisema migogoro ya ardhi ni mikubwa na kwamba wanatoa msaada huo bila malipo.

Maswi amesema kwa kuwa wanaendelea kutoa huduma wanatarajia idadi hiyo itaongezeka na kwamba wana mkakati na mpango wa kuweza kusambaa katika mikoa mingine ambayo hawajafika ambapo watatoa taarifa katika mikoa ambayo wataanza kusambaa kutoa msaada huo kwa watanzania wengine.

Dk. Maswi amempongeza Dk. Samia suluhu Hassan kwa kukubali kutumia jina lake kusaidia watanzania kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Amesema kuwa wapo katika maonesho hayo ili kuhakikisha wanatoa huduma ya usaidizi kwa watanzania watakaofika na kuhitaji huduma hiyo kutoka wizarani kwao ambapo wanasaidia na kusimamia upande wa mirathi na Ardhi.

"Mama Samia ametoa nafasi hii tutoe huduma ya msaada wa kisheria bila malipo kwa watanzania, huduma hii ni kubwa kwa sasa tunapaswa kuisambaza katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar," ameeleza.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa tayari wameshazunguka mikoa Saba ya awali huku akisema wana mpango wa kufika mikoa mingine 10 kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kutoa usaidizi wa watanzania wenye matatizo katika Sheria.

Amefafanua kuwa kuna wengine wanahitaji msaada wa kisheria huku akisema Rais Dk Samia amesema yupo tayari kutoa msaada huo wa kisheria.

Post a Comment

0 Comments

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA