MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO WAJUMBE WA NaCONGO NA WASAJILI WASAIDIZI YAFUNGULIWA

Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeandaa mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Taifa Mashirika Yasiyo ya kiserikali (NaCONGO),na Wasajili Wasaidizi kwa ngazi ya mikoa na Halmashauri zote nchini lengo likiwa ni kuwapitisha katika Sheria,Kanuni na Miongozo, mfumo wa Kieletroniki wa usajili na uratibu (NIS).

Mafunzo hayo, yameandaliwa na Wizara hiyo kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hayo yamesemwa leo Septemba 4, 2024 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu wakati akifungua mafunzo hayo ya siku mbili ameeleza kuwa 

Wizara inatambua kuwa kuna changamoto mbalimbali katika uratibu yakiwamo ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu mfumo wa NIS ambao umefanyiwa mabadiliko hasa baada ya kuongezewa kipengele cha Ramani ya Kidigitali.

Mdemu amesema kuwa kutokana na kuboreshwa kwa mfumo huo baadhi ya taarifa zitahitajika kuhuishwa katika mfumo wa NIS.

Amefafanua kuwa taarifa za Mashirika katika maeneo yao zinahitajika kuhuishwa na kuingiza taarifa za Vikundi vya kijamii (CBOs),katika mfumo huu.

"Wizara inatarajia baada ya Mafunzo haya mtakuwa na ufanisi katika utendaji kazi wenu katika uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Hii itasaidia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuzingatia Sheria katika utendaji kazi wake ikiwa ni pamoja na ulipaji wa ada, utumaji wa taarifa na mikataba ya fedha," amesema.

Ameongeza kuwa wanatarajia kutaongezeka kwa uwazi na uwajibikaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na yatajikita katika kuzingatiaji mila na desturi za mtanzania na kuhakikisha miradi inayotekelezwa inanufaisha jamii inayolengwa ili kuleta maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika hayo Mwantumu Mahiza amewataka Wasajili kufanya kazi kwa karibu na NGOs kwenye maeneo yao na kufuatilia shughuli wanazofanya kwa mustakabali wa nchi ya Tanzania.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Serikali (NaCONGO) Makala Jasper ameishukuru Wizara kwa ushirikiano inaotoa kwa mashirika yote nchini katika ngazi zote.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI