📍Serikali kuendeIea kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameweka wazi kuwa Tanzania haitoruhusu biashara ya dawa za kulevya na kwamba huku akitoa onyo kali kwa wauzaji, wasambazaji, watumiaji, na walimaji wa dawa za kulevya.
Hayo ameyasema leo, Juni 26,2025 wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Dawa za Kulevya Duniani, alisema Tanzania siyo mahali salama kwa wauzaji, wasafirishaji, walimaji, wala watumiaji wa dawa za kulevya. Tumeiva na sasa tunaenda kukomesha biashara hiyo.
Hata hivyo Waziri Mkuu Majaliwa alihamasisha vyombo vya ulinzi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Alisema kazi kubwa ya uwekezaji kwenye eneo hilo imefanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye ameongeza bajeti ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na kuwapatia vyombo vya usafiri ili wafanye kazi yao kwa ufanisi zaidi.
Waziri Majaliwa aliongeza kuwa matumizi ya dawa za kulevya zina madhara makubwa kwani zinapoteza uwezo wa mwili na uwezo wa kiakili wa kufikiri mambo.
"Ufanisi mkubwa unaoonekana hivi sasa unatokana na kufungamanishwa kwa Mamlaka ya DCEA ya Tanzania Bara na ile ya ZDCEA ya Zanzibar ambazo zinafanya kazi kwa karibu," alisema Waziri Mkuu.
Awali, Naibu Waziri wa Nchi (OWM – Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderianga alisema Ofisi ya Waziri Mkuu imeongeza operesheni na usimamizi kwa kufungua ofisi za kanda ambapo mkoa wa Dodoma tayari unayo ofisi ya Kanda.
"Rais Samia ameweka fedha nyingi na vifaa ili kuhakikisha anawaokoa vijana wa Kitanzania kutoka kwenye matumizi ya dawa za kulevya," alieleza.
Naye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alisema kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kimataifa Tanzania iko vizuri.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alieleza kuwa wamekamata dawa za kulevya jumla ya kilogramu 2,301,414.94 katika kipindi hiki huku akisema akiasi hicho ni kikubwa ikilingalishwa na kilo 2,050,542.73 zilizokamatwa kati ya Juni, 2023 na Mei, 2024.
"Kutokana na uongozi madhubuti wa Serikali ya awamu ya sita, kwa kipindi cha kuanzia Juni, 2024 hadi Mei, 2025, kumekuwa na ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya ukilinganisha na miaka iliyopita," alisema.
Alifafanua kuwa kuanzia Januari hadi Desemba 2024, jumla ya kilo 2,327,983.8 zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 1,965,341 zilizokamatwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2023.
0 Comments