Na WMJJWM- Morogoro
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ameitaka jamii kuwawezesha watu wenye ulemavu ili waweze kuishi kwa amani na kushiriki katika maendeleo na kuzifikia haki zao za msingi.
Wakili Mpanju ameyasema hayo tarehe 3 Desemba 2025 katika Maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Kitaifa yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Waislam mkoani wa Morogoro.
Amesema watu wenye ulemavu nchini ni takribani asilimia 11.2 ya watanzania wote hivyo ni idadi kubwa inayohitaji ulinzi na uwezeshaji mkubwa ili waweze kushiriki katika maendeleo.
Aidha, Wakili Mpanju amesisitiza viongozi wa dini, viongozi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii, wasanii, viongozi wa vyama vya siasa na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi kudumisha amani ya Tanzania huku akiwataka watanzania kudumisha amani, umoja na ushirikiano kwa kuwa ndizo tunu zitakazopelekea kufikia maendeleo ya nchi.
"Maneno yetu, matendo yetu tunapokuwa kwenye majukwaa na maeneo mbalimbali kadri Mungu anavyotujalia tuhimize amani na mshikamano tukijua uwepo wa amani ni msingi wa maendeleo thabiti kwa Taifa. Lakini msingi huu unaotoa fursa kwa kila mtanzania kuweza kushiriki kwenye maendeleo na kunufaika na haki nyingine za msingi na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.
Amewataka wazazi wa watoto wenye ulemavu kuwatoa watoto wao ili wapate elimu itakayotusaidia kushiriki kwenye maendeleo kupitia ajira na kuwekeza kwenye shughuli mbalimbali na kuchangia maendeleo ya familia zao na Taifa.
"Niwapongeze viongozi wa SHIVYAWATA, viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu pamoja na asasi za watu wenye ulemavu kwa kufanya kazi kubwa ya kuweza kuwasemea na kuwafikia watu wenye ulemavu popote walipo." amesisitiza Wakili Mpanju
Awali akizungumza katika Maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amezitaka Halmashauri mkoani humo kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya kwa kundi la watu wenye ulemavu.
Aidha Mhe Malima amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye ulemavu nchini katika nyanja zote ikiwemo elimu, afya, uwezeshaji wa kiuchumi, huduma za marekebisho, michezo, kiutamaduni pamoja na shughuli za kisiasa.
"Katika kutekeleza hili Serikali imeboresha miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wenye ulemavu kwa kujenga mabweni mahsusi katika mikoa ya Shinyanga, Njombe, Arusha, Lindi, Tabora, Singida, Manyara na Rukwa pamoja na kuhakikisha mahitaji yote ya msingi ikiwa pamoja na vifaa vya kujifunzia na nyenzo za kujilinda."amesisitiza Mhe. Malima
Pia amesema katika kutekeleza hilo kumeandaliwa na Miongozo mbalimbali ikiwemo Muongozo wa Mafunzo ya Amali kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum (2025) ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanakuwa na maarifa na stadi zitakazowezesha kujitegemea na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Amesema Serikali imeendelea kutenga fedha za ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/25 zaidi ya shilingi milioni 238 kilitolewa kwa vyama 13 na Shirikisho la SHIVYAWATA.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya watu wenye Ulemavu Tanzania SHIVYAWATA Hamadi Abdallah amesema Serikali haina budi kufanya mapitio ya Sera inayohusu watu wenye ulemavu pamoja na mwongozo wa Taifa wa Ufikivu ambapo itachangia ujenzi wa jamii jumuishi ya watu wenye ulemavu.








0 Comments