UIMARISHAJI WA MIFUMO YA UFUATILIAJI WA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO NI KIPAUMBELE CHA SERIKALI-WAKILI MPANJU


Na Witness Masalu WMJJWM-Morogoro

SERIKALI inaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuhakikisha wadau wote wenye jukumu la kuhakikisha watoto wanakua na kufikia utimilifu wao.  

Hayo yamebainishwa leo 04, Novemba 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju wakati akifungua rasmi mafunzo ya kadi ya alama (scorecard kwa Maafisa Ustawi wa Jamii, Elimu na Lishe pamoja na waratibu wa afya ya Mama na Mtoto kutoka Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini.  

Wakili Mpanju amesema kadi hiyo ya alama itawezesha kuunganisha sekta zote na kufanya kazi kwa pamoja hivyo kumlazimu kila mtu kutekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa. 

“Tumepata nyenzo ya Kitaifa itayoweza kutusaidia kufuatilia mienendo ya mtoto kuanzia ujauzito, kuzaliwa, ukuaji na ulinzi wake mpaka kufikia hatua ya elimu na inaleta sekta zote kwa pamoja na hii si nyenzo ya kawaida” amesema Wakili Mpanju.

Vilevile Wakili Mpanju amefafanua kwamba kadi hiyo ya alama itasaidia Taifa katika kutambua mapungufu yaliyopo na kuja na afua stahiki za kumlinda mtoto katika jamii zote bila ubaguzi.

“Kadi ya alama (scorecard) itakuwa na maana endapo kila mtu atatimiza majukumu yake katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya halmashauri, Mkoa mpaka Kitaifa ili kuhakikisha kinakuwa na chombo kitachowezesha Taifa katika kuweka mipango, bajeti pamoja na afua zinazokuza na kustawisha malezi, makuzi na Maendeleo ya Mtoto.” amesema Mpanju

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI Subisya Kabuje amesema kadi alama hiyo itatumika katika kupata taarifa sahihi pamoja na kuboresha maamuzi mbalimbali katika Serikali za mitaa na Tawala za Mikoa hivyo kutoa hamasa kwa wadau wote kutekeleza wajibu wao ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kuboresha huduma kwa ukuaji na ustawi wa watoto.

Naye  Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Mwajuma Kibwana ameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa taarifa katika uboreshaji wa huduma na kutoa hamasa kwa wadau wote kuwa mstari wa mbele ili kutimiza malengo ya Serikali.



Post a Comment

0 Comments

TAWA YAKABIDHI BWENI LA WASICHANA SHULE YA SEKONDARI MCHENGERWA, RUFIJI