SERIKALI YAPELEKA TABASAMU KWA WANAWAKE,VIJANA NA WENYE ULEMAVU MTWARA

Na Mwandishi wetu, Mtwara.

SERIKALI kupitia Ofisi ya Halmashauri ya Mtwara Mikindani yakabidhi kiasi cha shilingi milioni 342 ikiwa ni jitihada ya kujikita katika utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Mkoani Mtwara, Mkindani leo tarehe 14/02/2026 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga, amesema hatua hiyo ni hatua ya utekelezaji wa sera na mwelekeo wa maendeleo unaolenga kujenga uchumi jumuishi unaowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na maendeleo ya Taifa.

Naibu Waziri Ummy amefafanua, “Mikopo hiyo inalenga kuchochea na kuinua uchumi wa chini kwenda juu sambamba na dira ya Taifa ya kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2050.”

Ameongeza kusema, utoaji wa vifaa saidizi ikiwemo viti mwendo, magongo, fimbo za walemavu wa macho pamoja na taulo za kike, ni utekelezaji wa sera ya kutomwacha mtu nyuma katika safari ya maendeleo, sambamba na maono ya kitaifa ya kujenga jamii yenye heshima, utu na usawa wa fursa.

Kwa upande wake (Mb) Mtwara Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Dkt. Joel Arthur Nanauka, ameweka wazi kuwa Serikali katika jitahada za kuwakwamua wananchi kiuchumi itaendelea na utekelezaji wa kuleta wa miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Mtwara ikiwemo kuboresha Bandari ya Mtwara, ujenzi wa reli, na uboreshaji wa uwanja wa ndege pamoja na marekebisho ya miundombinu ya Barabara.

Waziri Nanauka amehimiza, “Wanufaika wa mikopo hiyo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, na kurejesha kwa wakati ili kushirikiana katika kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwao binafsi na Taifa kwa ujumla.”





Post a Comment

0 Comments

SERIKALI YAPELEKA TABASAMU KWA WANAWAKE,VIJANA NA WENYE ULEMAVU MTWARA