📍Serikali Yaongeza Kasi Kuboresha Huduma
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
MAJI ni rasilimali muhimu kwa uhai wa viumbe wote duniani. Bila maji, maisha hayawezi kuwepo kwani hutumika katika shughuli mbalimbali zikiwemo kunywa, kilimo, uzalishaji wa nishati na usafi wa mazingira.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imeeleza mafanikio makubwa ya mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ikionyesha jitihada za dhati za Serikali katika kuhakikisha huduma bora za maji zinawafikia wananchi kwa usawa na kwa wakati.
Mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia uwekezaji mkubwa ulioboreshwa katika sekta ya maji.
Mnamo Machi 19 mwaka huu, EWURA ilizindua rasmi Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa fedha 2024/2025, tukio lililoambatana na mjadala wa kitaalamu pamoja na tathmini ya utendaji wa mamlaka 83 za maji nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, anasisitiza kuwa sekta ya maji ni kiini cha maendeleo endelevu ya Taifa huku akiishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kuboresha huduma za maji.
“Taarifa ya mwaka 2024/2025 inachambua utendaji wa mamlaka za maji kwa kutumia vigezo vya EWURA vya Upimaji wa Utendaji (2022), huku ikitoa mapendekezo ya kuboresha ufanisi na utoaji wa huduma,” anasema.
MATOKEO YA UTENDAJI
Kwa mujibu wa Dk. Andilile, mamlaka zilizo katika kiwango cha Bora Sana (Excellent) zimeongezeka kutoka asilimia 1 hadi 5. Hata hivyo, mamlaka zilizo katika kiwango cha Vizuri Sana (Very Good) zimepungua kutoka asilimia 20 hadi 11, hali inayoashiria baadhi ya mamlaka kupanda hadi kiwango cha juu zaidi.
Aidha, anasema mamlaka zilizo katika kiwango cha Vizuri (Good) zimeongezeka kutoka asilimia 38 hadi 46, zikionyesha kuimarika kwa utoaji wa huduma na kwamba mamlaka zilizo katika kiwango cha Wastani (Fair) zimepungua kutoka asilimia 39 hadi 35.
Kwa upande mwingine, anaeleza kuwa mamlaka zenye utendaji usioridhisha zimeongezeka kutoka asilimia 2 hadi 4.
MATOKEO MUHIMU
Dk. Andilile anabainisha kuwa uwezo wa miundombinu ya uzalishaji maji umeongezeka kwa asilimia 8, kutoka mita za ujazo milioni 736 hadi milioni 795.
Anasema uzalishaji wa maji umeongezeka kwa asilimia 19.3, kutoka mita za ujazo milioni 389 hadi milioni 464 ambapo maunganisho ya huduma ya maji yameongezeka kwa asilimia 9 na kufikia zaidi ya wateja milioni 1.8.
Akizungumzia mapato ya mamlaka za maji anaeleza kuwa yameongezeka kwa asilimia 14, kutoka shilingi bilioni 419.2 hadi bilioni 479.1, jambo linaloashiria kuimarika kwa usimamizi wa kifedha.
CHANGAMOTO ZINAZOHITAJI HATUA
Anafafanua kuwa licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto kadhaa zinazohitaji kushughulikiwa.
Mkurugenzi Mkuu huyo anasema moja ya changamoto kubwa ni upotevu wa maji (Non-Revenue Water - NRW), ambapo asilimia 42.3 ya maji hupotea, kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 20.
Pia, anaongeza kuwa uzalishaji wa maji haukidhi mahitaji, ambapo maji yanayozalishwa yanakidhi asilimia 52 pekee ya mahitaji na kwamba huduma ya maji hupatikana kwa wastani wa saa 14 kwa siku, hali inayodai maboresho zaidi.
"Changamoto nyingine ni ukosefu wa miundombinu ya kutibu majitaka na tope kinyesi, ambapo asilimia 71 ya mamlaka hazina miundombinu hii," anaeleza Dk. Andilile.
Pia Dk.Andilile anasema ukosefu wa hati miliki za ardhi kwa miundombinu ya maji unakwamisha ushiriki wa sekta binafsi.
Aidha, anaongeza kuwa kuna ucheleweshaji wa uwasilishaji wa tozo za udhibiti, ambapo shilingi bilioni 5.69 hazijawasilishwa kwa mujibu wa sheria.
NJIA ZA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO
Dk. Andilile anasisitiza umuhimu wa kubadili mtazamo wa utendaji kwa kutumia mbinu mpya (business unusual), ikiwa ni pamoja na kutafuta vyanzo mbadala vya fedha na kushirikisha sekta binafsi kupitia miradi ya ubia (PPP).
Pia, anasisitiza umuhimu wa kuzingatia utawala bora, kuongeza uwajibikaji wa bodi za wakurugenzi, pamoja na kupima utendaji wa menejimenti kwa matokeo.
UTOAJI WA TUZO
Katika mkutano huo, EWURA imetoa tuzo kwa mamlaka zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma.Kwa mamlaka zenye wateja zaidi ya 20,000, Moshi ilishika nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Songea nafasi ya pili na Iringa nafasi ya tatu.
Kwa kundi la mamlaka zenye wateja kati ya 5,000 na 20,000, Nzega ilishika nafasi ya kwanza, Igunga ya pili, huku Geita ikishika nafasi ya tatu bila kupata tuzo kutokana na kutofikia viwango vinavyotakiwa.
Kwa mamlaka zenye wateja chini ya 5,000, Biharamulo ilishika nafasi ya kwanza, Mpwapwa ya pili na Kibondo ya tatu.
KAULI YA WAZIRI WA MAJI
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akizindua rasmi taarifa hiyo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote ili kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira.
Anasema Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa mfumo wa kimkakati wa usambazaji maji wa Taifa (National Water Grid), utakaosaidia kuunganisha vyanzo vikuu vya maji na maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Waziri huyo anasema mfumo huo unalenga kuhakikisha upatikanaji wa maji mwaka mzima, kupunguza utegemezi wa vyanzo visivyo vya kudumu na kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Anaeleza kuwa Serikali imeweka bayana dhamira yake ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi, salama na ya uhakika kwa gharama nafuu, huku ikisisitiza uwajibikaji, uwazi na ufanisi kwa mamlaka zote za maji nchini.

.jpg)

0 Comments