📍Wananchi Kunufaika na Huduma za Kisheria Kupitia Contact Center ya Wizara
Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WIZARA ya Katiba na Sheria imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi kwa kuanzisha Kituo cha Huduma kwa Mteja (Contact Center), mfumo wa kisasa unaorahisisha upokeaji wa malalamiko, utoaji wa msaada wa kisheria na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Serikali na wananchi.
Kupitia kituo hicho, wananchi kwa sasa wanapata fursa ya kusikilizwa, kuhudumiwa na kupatiwa ufumbuzi wa changamoto zao kwa haraka bila vikwazo vya umbali wala gharama.
Katika jitihada za kuimarisha upatikanaji wa haki na kurahisisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, Wizara hiyo imechukua hatua madhubuti kwa kuanzisha kituo hicho ambacho kimekuwa daraja muhimu la kusikiliza, kushughulikia na kutatua changamoto za kisheria kwa wakati.
Kituo hicho kinatajwa kuwa suluhisho la kisasa linaloweka mbele haki, uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria nchini.
Kwa mujibu wa majukumu yake yaliyoainishwa kupitia Hati Idhini ya Mgawanyo wa Majukumu ya Wizara (Tangazo la Serikali Na. 619A la Agosti 30, 2023), pamoja na Sheria ya Mawaziri, Wizara ya Katiba na Sheria ina wajibu wa kusimamia na kuwezesha mfumo wa haki.
Ili kutekeleza jukumu hilo kwa vitendo, Wizara hiyo ilianzisha kituo hicho chenye lengo la kutoa msaada wa kisheria, kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi, pamoja na kukusanya maoni na ushauri kwa ajili ya kuboresha huduma.
UANZISHWAJI WA KITUO
Uanzishwaji wa kituo hicho ni matokeo ya utekelezaji wa Programu ya Kujenga Uwezo wa Taasisi katika Kupambana na Rushwa (BSAAT), inayoratibiwa na Ofisi ya Rais – Ikulu kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza.
Kituo kilianza kazi Februari 14, 2024 na baadaye kuzinduliwa rasmi Septemba 5, 2024, kikishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Lengo kuu la uzinduzi lilikuwa kulitambulisha rasmi kwa umma, kueleza huduma zake na kuonesha namna kinavyorahisisha upatikanaji wa huduma za Wizara bila wananchi kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Hatua hiyo inaendana na Mkataba wa Huduma kwa Mteja wa mwaka 2020 unaosisitiza utoaji wa huduma kwa haki na kwa wakati.
Kituo kinatoa huduma mbalimbali ikiwemo msaada wa kisheria kwa wananchi wasiomudu gharama za mawakili, pamoja na kupokea maoni, mapendekezo na ushauri kuhusu huduma za Wizara.
Ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, kituo hicho kinatumia njia mbalimbali za mawasiliano zikiwemo simu za bure na za kawaida, WhatsApp, barua pepe pamoja na posta.
UTENDAJI KAZI WAKE
Kwa upande wa utendaji, kituo kinatumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA ikiwemo mfumo wa Contact Center kwa mawasiliano ya simu na Customer Relationship Management (CRM) kwa ajili ya kuhifadhi na kuchakata taarifa za wateja, pamoja na mfumo wa kuunganisha mitandao ya kijamii.
Mifumo hiyo imeongeza ufanisi katika kupokea na kufuatilia malalamiko ya wananchi kwa usahihi zaidi.
Huduma katika kituo hutolewa kwa ngazi tatu: ngazi ya kwanza ni maafisa huduma (Agents) ambao ni wanasheria waliopatiwa mafunzo maalum; ngazi ya pili ni msimamizi (Supervisor); na ngazi ya tatu ni idara husika zinazoshughulikia masuala maalum.
Mfumo huu umewezesha kushughulikia kwa ufanisi masuala yanayowasilishwa na wananchi.
Tangu kuanzishwa kwake, kituo kimeonyesha mafanikio makubwa ambapo hadi Desemba 31, 2025 kimepokea malalamiko 1,915; kati ya hayo, 1,327 yameshatatuliwa huku mengine yakiendelea kufanyiwa kazi.
Aidha, kimepunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma na kuongeza kasi ya upatikanaji wa mrejesho wa malalamiko.
USHIRIKIANO NA TAASISI NYINGINE
Ushirikiano kati ya Wizara na taasisi nyingine za umma umeimarika kupitia kituo hicho, ambapo taasisi kama Mahakama ya Tanzania, Jeshi la Polisi, TAKUKURU na Wizara ya Afya zimekuwa zikishirikiana kushughulikia masuala ya wananchi kwa haraka na ufanisi.
Kwa sasa, kituo kinaendeshwa na watumishi 10, wakiwemo wanasheria tisa na mtaalamu mmoja wa TEHAMA, ambao hupatiwa mafunzo endelevu ili kuhakikisha utoaji wa huduma unazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna mahitaji ya kupanua miundombinu na kuongeza rasilimali watu ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya huduma.
KUIMARISHA HUDUMA
Katika kuimarisha zaidi huduma, Wizara imeweka mipango ya kuboresha kituo kupitia bajeti ya mwaka 2025/2026, ikiwemo kuhamia katika ofisi ya kisasa na kuongeza uwezo wa kiteknolojia.
Kuanzishwa kwa Kituo cha Huduma kwa Mteja ni hatua kubwa inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi, kulinda haki zao na kuhakikisha wanapata huduma bora kwa wakati.
Inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2026, kituo hicho kitakuwa mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine za Serikali katika utoaji wa huduma kwa umma.
UZINDUZI WA PROGRAMU YA "SEMA NA WAZIRI"
Machi 17, 2026, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ilizindua rasmi programu ya “Sema na Waziri” yenye lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi na kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na jamii.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, anasema programu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha na kuboresha vituo vya huduma kwa mteja serikalini ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Anaeleza kuwa kupitia kituo hicho, wananchi watapata fursa ya kuwasilisha malalamiko, kuuliza maswali na kupata ushauri wa kisheria kwa urahisi zaidi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kama ilivyokuwa awali.
“Programu hii inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msaada wa kisheria kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi,” anasema Dk. Homera.
Anabainisha kuwa kupitia programu hiyo, wananchi wataweza kuwasilisha changamoto mbalimbali za kisheria ikiwemo mirathi, ardhi, kazi na ajira, mikataba, ndoa na talaka, jinai, ukatili wa kijinsia, matunzo ya watoto pamoja na madai.
Aidha, anasema programu hiyo inalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika kuboresha huduma zinazotolewa na Wizara.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara inatarajia kupokea takribani wananchi laki mbili kwa mwezi kupitia kituo hicho, hatua itakayowezesha zaidi ya Watanzania milioni 2.4 kupata huduma za msaada wa kisheria kwa mwaka.
Anaongeza kuwa Wizara imepanga kuendesha kampeni ya kitaifa ya kutangaza huduma za kituo hicho katika mikoa yote ya Tanzania Bara ili kuongeza uelewa na kuhamasisha matumizi ya huduma hizo.
Aidha, anawataka wananchi kutumia fursa hiyo kwa kuwasiliana kupitia namba 0262 160 360 au 0800 004 004 ili kupata huduma na msaada wa kisheria kwa haraka na ufanisi.




0 Comments