SERIKALI YAPANGA KUONGEZA UZALISHAJI WA MKONGE HADI TANI 80,000 MWAKA 2026/2027


Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao la mkonge nchini kutoka tani 64,321.77 zilizofikiwa hadi Machi 2026 hadi kufikia tani 80,000 katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha zao hilo kimkakati na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

Hayo yamesemwa leo Aprili 28,2026 bungeni na Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, amesema kuwa juhudi hizo zitatekelezwa kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Amesema katika kufanikisha lengo hilo, Wizara itasambaza miche ya mkonge milioni 3.5 kwa wakulima pamoja na kutoa mafunzo ya uzalishaji na uongezaji thamani kwa wadau 200 na maafisa ugani 50 kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Aidha, Chongolo ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mkonge kwa kununua na kusimika mashine 10 za kuchakata mkonge (dikotiketa), zenye uwezo wa kuchakata tani mbili kwa siku, zitakazosambazwa katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Shinyanga na Tabora.

Ameongeza kuwa ujenzi wa vituo viwili vya kuchakata mkonge katika wilaya za Mkinga na Handeni unaendelea kukamilishwa sambamba na kuanzishwa kwa vituo 13 vya ukusanyaji na uuzaji wa mkonge kwa wakulima wadogo ili kurahisisha upatikanaji wa masoko.

"Wizara itaweka miundombinu ya uongezaji thamani ikiwemo brushing na baling katika mikoa ya Singida, Pwani na Tanga pamoja na kukamilisha ujenzi wa ghala, ofisi na miundombinu ya maji taka katika viwanda vya Taula na Kibaranga," amesema Waziri huyo.

Akizungumzia mafanikio ya mwaka 2025/2026, Chongolo amesema hadi kufikia Machi 2026 uzalishaji wa mkonge umefikia asilimia 80.4 ya lengo la tani 80,000, hali inayotokana na juhudi za kutoa mafunzo kwa wadau 6,853 na maafisa ugani 44 katika mikoa mbalimbali nchini.

Amebainisha kuwa Serikali pia imefanikiwa kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja ya wakulima wadogo yenye ukubwa wa hekta 9,211 pamoja na kuwezesha umiliki wa ardhi ya kilimo yenye ukubwa wa hekta 21,625.5, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 120,000 ifikapo mwaka 2030.

Katika kuimarisha zaidi sekta hiyo, Chongolo amesema tayari kiwanda kimoja cha kuchakata mkonge chenye uwezo wa kuchakata tani tano kwa siku kimeanzishwa mkoani Tanga, huku maandalizi ya kuanzisha viwanda vingine viwili katika wilaya za Handeni na Mkinga yakiendelea.

Ameeleza kuwa Serikali imewezesha usajili wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Mkonge Mkoa wa Tanga (Tanga Sisal Cooperative Union Ltd), kitakachosaidia kuratibu shughuli za vyama vya msingi na kuboresha masoko ya zao hilo.

Katika hatua ya kuongeza thamani ya zao la mkonge, amesema Wizara inaendelea na ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa nzi chuma (Black Soldier Flies), kwa kutumia mabaki ya mkonge ili kuzalisha protini kwa ajili ya mifugo, sambamba na kuendelea na taratibu za kurejesha viwanda na mashamba yaliyokuwa chini ya Kampuni ya Sisalana.

Hatua hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kulifufua zao la mkonge na kulifanya kuwa chanzo kikuu cha ajira, kipato na maendeleo kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments

PURA YAIMARISHA USIMAMIZI WA MAFUTA NA GESI, SERIKALI YALENGA KUVUTIA UWEKEZAJI ZAIDI