Na Asha Mwakyonde,DODOMA
SEKTA ya mafuta na gesi asilia nchini imeendelea kushika nafasi ya kimkakati katika kukuza uchumi wa taifa, huku Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ikibeba jukumu muhimu la kuhakikisha rasilimali hizo zinasimamiwa kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia maslahi ya Watanzania.
Kupitia usimamizi wa shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji, PURA imekuwa nguzo kuu katika kujenga mazingira thabiti ya uwekezaji na kuhakikisha nchi inanufaika ipasavyo na utajiri wake wa nishati.
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha usimamizi na udhibiti wa shughuli za mafuta na gesi asilia nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kukuza sekta ya nishati na kuvutia uwekezaji wa kimkakati.
Akiwasilisha bungeni hivi karibuni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Wizara hiyo, Deogratius Ndejembi, anaeleza kuwa kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia ili kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa manufaa ya taifa.
Anasema katika utekelezaji huo, Serikali imepanga kuandaa Mpango wa Tafiti za Awali katika maeneo yenye viashiria vya mafuta na gesi, kugawa maeneo katika vitalu vya utafutaji pamoja na kuandaa taarifa za kina za kijiolojia na kijiofizikia zitakazosaidia kuvutia wawekezaji.
Aidha, anafafanua kuwa tathmini za athari kwa mazingira na jamii zitaendelea kufanyika ili kulinda ustawi wa wananchi na mazingira kwa ujumla.
Waziri Ndejembi anasema juhudi hizo pia zitaenda sambamba na ushiriki wa Tanzania katika maonesho na makongamano ya kimataifa ya mafuta na gesi, ikiwa ni mkakati wa kufanikisha Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu vya Utafutaji.
"Kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizi, jumla ya shilingi bilioni 4 zimetengwa," anasema.
Akizungumzia mafanikio ya sasa, anasema hadi kufikia Machi 2026, PURA imefanikiwa kusimamia uzalishaji thabiti wa gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay na Songo Songo, hali inayochangia upatikanaji wa nishati kwa matumizi mbalimbali nchini.
Aidha, anasema PURA imeendelea kusimamia uchorongaji wa visima vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay, ambapo kisima kimoja tayari kimekamilika na kipo katika hatua ya uzalishaji wa majaribio huku visima viwili vilivyosalia vikiendelea kuchorongwa.
"Kwa upande wa utafiti, kazi za uchukuaji wa takwimu za mitetemo zinaendelea katika vitalu vya Eyasi ,Wembere na Lindi,Mtwara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kubaini rasilimali mpya za mafuta na gesi," anasema.
Akizungumzia kuimarisha uwazi na ufanisi wa mikataba ya sekta hiyo, anaeleza kuwa PURA imeendelea kufanya ukaguzi wa gharama na mapato katika mikataba ya Ugawanaji Mapato (PSA) kati ya Serikali na wawekezaji 11.
Waziri Ndejembi anabainisha kuwa tangu mwaka 2017, Serikali imefanikiwa kuokoa shilingi bilioni 322 zilizokuwa zinadaiwa na wawekezaji na kurejeshwa katika mfuko wa ugawanaji mapato.
Anaeleza kuwa Sambamba na hilo, Serikali kupitia PURA imeendelea kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi kwa kushiriki makongamano ya kimataifa, yakiwemo yaliyofanyika Afrika Kusini na Ghana, kwa lengo la kuwavutia wawekezaji zaidi kabla ya uzinduzi wa duru mpya ya vitalu vya utafutaji.
Kwa upande wa udhibiti wa sekta nzima ya nishati, anafafanua kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi kupitia PURA kwa mkondo wa juu wa petroli na EWURA kwa mkondo wa kati na chini, hatua inayolenga kuhakikisha huduma za nishati zinatolewa kwa kuzingatia sheria, ubora na maslahi ya wananchi.
Anaongeza kuwa hatua hizo zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuifanya sekta ya nishati kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa taifa kupitia usimamizi imara, uwazi na mazingira rafiki ya uwekezaji.
WIKI YA NISHATI BUNGENI
Akizungumza katika wiki ya Nishati iliyoenda Sambamba na maonesho ya bidhaa mbalimbali wakati akitoa taarifa Kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, anayeshughulikia mafuta na gesi asilia,Dk.James Mataragio alipotembelea Banda la Mamlaka hiyo katika wiki ya Nishati katika viwanja vya Bunge.
Mamlaka hiyo Mkuu wa Kitengo Cha Uhusishwaji Wa wazawa na wadau kutoka PURA,Charles Nyangi anasema PURA imekamilisha uchimbaji wa kisima kimoja cha uchimbaji gesi cha Mnazi Bay Mtwara ambacho kimeonesha maajabu kwa kuwa na uwezo wa kuzalisha gesi futi za ujazo milioni 45 Kwa siku.
Anasema uchimbaji wa visima ni hatua iliyokuwa ikitekelezwa na Mamlaka hiyo na kwamba kisima hicho kilichokamilika awali kilitarajiwa kuzalisha futi za ujazo milioni 20 Kwa siku jambo ambalo limekuwa ni tofauti na matarajio.
“Imekuwa ni mshangazo mkubwa kwetu, na hii ndio inaonyesha kuwa ipo akiba kubwa ya gesi nchini,” amesema Nyangi na kuongeza kuwa kisima lingine linaendelea na hatua za uchimbaji.
Anasema kisima hicho kimebakia mita 1500 kukamilika na kwamba hatuabalimbali za utafiti wa gesi zinaendelea katika mikoa ya Lindi na Mtwara huku akisema ipo akiba kubwa ya gesi,ikiwa ni baada ya kukamilika.


0 Comments