Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WANANCHI, wajasiriamali, wakulima na wafugaji wametakiwa kutumia fursa mbalimbali za mikopo na elimu ya fedha zinazotolewa na Mfuko wa SELF (SELF Microfinance Fund), ili kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Hayo yamesemwa leo Juni 18, 2026 na Meneja wa Mfuko wa SELF Kanda ya Kati, Aristid Tesha katika wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Tesha amesema kanda hiyo inahudumia mikoa ya Dodoma na Singida na kwamba mfuko huo unashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi na kuwaeleza fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.
Amesema tangu kuanza kwa maonesho hayo Juni 16, wananchi wengi wamejitokeza kutembelea banda la SELF kwa ajili ya kupata elimu kuhusu ujasiriamali, usimamizi wa fedha pamoja na huduma za mikopo zinazotolewa na mfuko huo.
“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu fursa zilizopo, hususan mikopo inayoweza kuwasaidia kukuza biashara zao, kuboresha makazi yao na kuendeleza shughuli za uzalishaji,” amesema Tesha.
Tesha amefafanua kuwa SELF inatoa aina mbalimbali za mikopo ikiwemo mikopo ya mtu mmoja mmoja kwa wajasiriamali wanaojihusisha na shughuli halali za kiuchumi, mikopo ya watumishi wa umma pamoja na mikopo ya jumla kwa taasisi zinazowakopesha wajasiriamali wadogo nchini.
Aidha, amesema mfuko huo una matawi 12 yanayohudumia Tanzania Bara na Zanzibar, jambo linalowezesha huduma zake kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa Tesha, SELF pia imeweka mkazo katika utoaji wa mikopo kwa sekta ya nishati safi na nishati mbadala, ikiwemo biashara za gesi, mifumo ya umeme wa jua (solar) na vifaa vinavyochangia utunzaji wa mazingira.
Ameeleza kuwa mikopo hiyo hutolewa kwa masharti nafuu ili kuwahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi kuingia katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira.
“Tunaendelea kuhamasisha wananchi wanaojihusisha na biashara za nishati safi kufika katika banda letu au ofisi zetu ili wapate maelezo ya namna ya kunufaika na mikopo hii yenye riba nafuu,” amesema.
Tesha ameongeza kuwa mfuko huo pia unatoa mikopo ya jumla kwa vyama vya ushirika, SACCOS na taasisi ndogo za fedha zinazowahudumia wananchi wa maeneo ya vijijini, hususan wakulima na wafugaji.
Amesema kupitia mikopo hiyo, taasisi mbalimbali zimefanikiwa kuwafikia wananchi wa maeneo ya pembezoni kwa kuwapatia mitaji na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.
Mbali na hilo, ameeleza kuwa SELF inatoa mikopo ya kuboresha makazi kwa wananchi wanaotaka kukamilisha ujenzi wa nyumba zao au kufanya ukarabati wa makazi yaliyopo.
Akizungumzia sekta ya kilimo na mifugo, Tesha amesema wakulima, wafugaji, vikundi vya kijamii pamoja na taasisi za kifedha zinazohudumia sekta hizo wanaweza kupata mikopo maalumu inayolenga kuimarisha minyororo ya thamani katika uzalishaji.
Amesema mfuko huo unatoa huduma mbalimbali za bima ikiwemo bima za vyombo vya moto, nyumba na mali nyingine, sambamba na kutoa elimu ya bima kwa wananchi.
Amewahimiza wananchi wa Dodoma na mikoa jirani kutembelea banda la SELF katika Viwanja vya Chinangali ili kujifunza zaidi kuhusu huduma na fursa zinazotolewa na mfuko huo kwa maendeleo ya kiuchumi ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

0 Comments