Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
JITIHADA za Serikali za kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala zimeendelea kuzaa matunda, baada ya mgogoro wa malipo wa Shilingi milioni sita kati ya Kampuni ya Core Mult General Supply Limited na mkandarasi mdogo, Sehewa Chando, kumalizika kwa maelewano
ya njia mbadala (ADR),kupitia wataalamu wa Wizara ya Katiba na Sheria,bila kufikishwa mahakamani.
Hayo yamejidhihirisha jana baada ya mgogoro wa malipo kati ya Kampuni ya Core Mult General Supply Limited na mkandarasi mdogo, Sehewa Chando, kufikiwa muafaka kupitia wataalamu wa Wizara ya Katiba na Sheria waliopo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF),'Sabasaba'.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Core Mult General Supply Limited, Tanziru Mkakile, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kupitia huduma zinazotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Alieleza kuwa kampuni yake ilimpa Chando kazi ya uchapishaji wa maandishi na nembo kwenye magari 200 ya Kampuni ya Dangote kwa makubaliano ya malipo ya jumla ya Shilingi milioni 54.
Mkakile alisema kampuni ilifanikiwa kumlipa Shilingi milioni 48, huku deni la Shilingi milioni sita likisalia kutokana na changamoto za kifedha zilizokuwa zimeikumba kampuni hiyo.
"Nilimwomba avute subira kwa kuwa ofisi ilikuwa inapitia changamoto za kifedha, lakini aliona tunamchelewesha ndipo akaamua kutafuta msaada wa kisheria," alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria walipokelewa vizuri na kupewa nafasi ya kusikilizwa, jambo lililowasaidia kufikia makubaliano ya kumaliza mgogoro huo kwa amani.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kampuni italipa deni la Shilingi milioni sita kwa awamu nne za Shilingi milioni 1.5 kila mwisho wa mwezi hadi deni litakapokamilika ndani ya miezi minne.
"Hadi sasa tumefikia makubaliano mazuri na mzee amekubali utaratibu huo. Tunamshukuru Mungu tumemaliza mgogoro huu kwa amani," alisema Mkakile.
Kwa upande wake, Sehewa Chando alisema aliamua kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kutafuta suluhisho la kisheria bila kulazimika kufikisha shauri hilo mahakamani.
Alisema kampuni hiyo ilimchelewesha kumlipa Shilingi milioni sita baada ya kumaliza kazi waliyoafikiana ambapo kupitia usuluhishi uliofanywa na wataalamu wa wizara hiyo wamefikia makubaliano yanayoridhisha pande zote.
"Nimefurahi kwa sababu tumepokelewa vizuri na tumefikia makubaliano ambayo hayajamuumiza mtu kwa upande zote mbili.Tumekubaliana utaratibu wa malipo na tumesaini makubaliano hayo," alisema Chando.
Naye Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Sylvester Zakayo, alisema wizara inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kisheria kwa wananchi, ikiwemo elimu ya sheria na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.
Alisema katika kipindi cha maonesho hayo, wizara imefanikiwa kusuluhisha migogoro mbalimbali, ukiwemo mgogoro kati ya Kampuni ya Core Mult General Supply Limited na mdai wake, Sehewa Chando.
Zakayo alibainisha kuwa baada ya kuwasikiliza wahusika kwa makini, waliweza kufikia makubaliano yaliyomaliza mgogoro huo bila kufika mahakamani.
Alihimiza wananchi na wafanyabiashara kuchagua utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kwa kuwa ni wa haraka, wenye gharama nafuu, huhifadhi siri za wahusika na husaidia kuendeleza mahusiano ya kibiashara hata baada ya mgogoro kumalizika.
Wakili Zakayo alieleza kuwa njia mbadala ya utatuzi wa migogoro ni suluhisho lenye manufaa makubwa kwa jamii na wafanyabiashara na kwamba hupunguza gharama, huokoa muda na hujenga mazingira ya kuendelea kushirikiana baada ya mgogoro kumalizika.




0 Comments