MTOTO WA MIAKA 14 AVUTIA WENGI VETA KWA KIPAJI CHA UPISHI, AOTA KUWA MPISHI WA KIMATAIFA


Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

Ndoto ya kuwa mpishi wa kimataifa ilianza kwa kutazama video za mapishi kupitia simu ya mama yake. Leo, akiwa na umri wa miaka 14 pekee, Said Mashauri, mwanafunzi wa Chuo cha VETA Njiro Arusha, ameibua mshangao kwa uwezo wake mkubwa wa kuandaa vyakula mbalimbali na kuwa mfano wa jinsi vipaji vinavyoweza kuendelezwa kupitia elimu ya ufundi na stadi.

Said amesema alivutiwa na taaluma ya upishi baada ya kuwaona wapishi wakubwa wakipika kupitia mitandao, hususan namna walivyokuwa wakirusha na kugeuza chapati kwa ustadi, jambo lililomfanya avutiwe na kuamua kufuata ndoto yake.

"Nikiwa nyumbani nilimuomba mama simu yake nikaanza kutazama video za mapishi mtandaoni. Nilipoona jinsi wapishi walivyokuwa wakipika, nilivutiwa sana na nikamwambia mama nataka kusomea masuala ya upishi," amesema Said.

Amesema alihitimu elimu ya msingi mwaka jana katika Shule ya Msingi Patandi iliyopo jijini Arusha, kabla ya kujiunga na Chuo cha VETA Njiro ili kujifunza taaluma ya upishi.

Kwa sasa, amesema analenga kuwa mpishi mkubwa wa kimataifa atakayefanya kazi katika hoteli mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, amewashauri watoto na vijana wenzake kutothamini taaluma za kawaida pekee, bali wajifunze pia fani za ufundi kama upishi, akieleza kuwa ni kazi yenye fursa nyingi za ajira na kujiajiri.

"Nawaomba watoto wenzangu wasione aibu kusomea upishi. Ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, na inaweza kukuwezesha kujiajiri hata kama hutapata ajira," amesema.

Kwa upande wake, mwalimu wa Uandaaji na Upishi wa Vyakula kutoka Chuo cha Utalii VETA Njiro Arusha, Robinson Mwaikuju, amesema Said ni miongoni mwa wanafunzi walioonyesha uwezo mkubwa ndani ya muda mfupi tangu aanze mafunzo.

Amesema mwanafunzi huyo amewashangaza walimu na wageni wengi wanaotembelea chuo kutokana na ubunifu na umahiri wake wa kuandaa vyakula mbalimbali.

"Hivi vyakula unavyoviona hapa ameviandaa yeye mwenyewe. Mimi ndiye mwalimu wake, lakini ndani ya miezi mitatu tu ameonyesha bidii kubwa na uwezo wa kujifunza kwa haraka," amesema Mwaikuju.

Ameongeza kuwa hatua ya Serikali kuendelea kuimarisha mafunzo ya amali na kuhamasisha ufundishaji wa masomo ya utalii na stadi mbalimbali kwa vijana itasaidia kukuza vipaji na kuongeza fursa za ajira.

Pia amewataka wazazi kuwahamasisha watoto wao kujiunga na VETA bila kujali umri wao, akisema elimu ya ufundi huwajengea uwezo wa kujitegemea mapema.

Mwaikuju amesema licha ya kuwa na umri wa miaka 14, Said tayari ana uwezo wa kupika pilau kwa idadi kubwa ya watu bila hofu na ameanza kujifunza maandalizi ya vyakula vya kimataifa, hatua inayomuweka kwenye msingi mzuri wa kutimiza ndoto yake ya kuwa mpishi wa kiwango cha kimataifa.

Post a Comment

0 Comments

TUTUBA: BODI YA BIMA YA AMANA, NGAO YA USALAMA WA FEDHA ZA WANANCHI