Na Asha Mwakyonde DAR ES SALAAM
SERIKALI imeanza kutekeleza Programu ya Matengenezo Endelevu ya Barabara kwa Kushirikisha Jamii (Community-Based Routine Maintenance CBRM), inayolenga kuboresha zaidi ya kilomita 15,000 za barabara nchini huku ikitoa fursa za ajira kwa zaidi ya vikundi 3,000 vya wananchi.
Akizungumza leo Julai 10,2026 kuhusu utekelezaji wa programu hiyo,Mshauri wa CBRM, Mhandisi Richard Missa, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), 'Sabasaba'amesema mpango huo unatekelezwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kwa ufadhili wa mkopo kutoka Benki ya Dunia, kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2025/2026 hadi 2027/2028.
Amesema lengo kuu la programu ni kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote kwa kufanya matengenezo ya kawaida yanayohusisha ushiriki wa vikundi vya wananchi wanaoishi karibu na barabara husika.
"Programu hii inalenga kushirikisha wananchi moja kwa moja katika matengenezo ya barabara huku ikiwapatia ajira na kipato. Tunataka barabara ziwe katika hali nzuri muda wote na jamii iwe sehemu ya kuzilinda," amesema Mhandisi Missa.
Mhandisi huyo ameeleza kuwa utekelezaji wa awamu ya kwanza tayari umeanza katika mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro na Dodoma, ambapo zaidi ya kilomita 1,500 za barabara zimeanza kuhudumiwa na vikundi 302 tayari vimenufaika kwa kupata kazi.
Kwa mujibu wa Missa, shughuli zinazofanywa na vikundi hivyo ni pamoja na kusafisha mifereji ya maji, kufungua makaravati na madaraja madogo, kuondoa vizuizi barabarani, kufyeka vichaka pembezoni mwa barabara na kuziba mashimo madogo yanayoweza kusababisha uharibifu wa miundombinu.
Amesema matengenezo hayo yanasaidia kuzuia maji ya mvua kuharibu barabara, hivyo kupunguza gharama za matengenezo makubwa na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za usafiri na usafirishaji katika kipindi chote cha mwaka.
Aidha, amesema programu hiyo inalenga kuongeza kipato cha wananchi wa maeneo husika kwa kuwapa fursa za ajira bila kuathiri shughuli zao nyingine za kiuchumi, kwani vikundi hupewa mikataba ya muda mrefu lakini hupangiwa ratiba inayowawezesha kuendelea na shughuli nyingine za uzalishaji.
Missa ameongeza kuwa pamoja na kushiriki katika matengenezo ya barabara, vikundi hivyo vinapatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili viweze kujiendesha na kuendelea kuwa imara hata vinapokosa kazi za matengenezo kwa muda.
Amesema programu hiyo pia inaunga mkono utekelezaji wa sera ya Serikali ya kutenga asilimia 30 ya fursa za manunuzi kwa makundi maalumu kupitia ushirikishwaji wa vikundi vya wananchi katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa CBRM haichukui nafasi ya wakandarasi wa kawaida wala wa mfumo wa Labour-Based, bali inaongeza ushiriki wa wananchi katika matengenezo ya kawaida yanayotumia nguvu kazi, wakati kazi zinazohitaji mitambo zinaendelea kutekelezwa na wakandarasi kama ilivyo kawaida.
Amesema Serikali inaamini kuwa kupitia programu hiyo, ubora wa barabara utaongezeka, ajira zitaimarika na wananchi watajenga utamaduni wa kulinda na kutunza miundombinu inayowahudumia kila siku.



0 Comments