TUTUBA AIPONGEZA IAA KWA KULEA WABUNIFU NA WAJASIRIAMALI KUPITIA KIATAMIZI CHA BIASHARA


Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, amepongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa mafanikio ya Kituo cha Kuatamia Biashara cha IAA (IAA Business Start Up Centre), akisema kimekuwa chachu ya kuwajengea vijana uwezo wa kubuni, kuanzisha na kukuza biashara zinazochangia maendeleo ya uchumi wa nchi.

Tutuba ametoa pongezi hizo Julai 10, 2026, alipotembelea banda la IAA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba.

Amesema anaamini kituo hicho kitaendelea kuwavutia vijana wengi zaidi kujiunga na chuo hicho kutokana na mchango wake katika kuwawezesha wanafunzi kujiajiri kupitia ubunifu na ujasiriamali.

"Ninaamini kuna vijana wengi watakaokuja kujifunza hapa, na wale waliopitia kituo hiki tayari wanatoa ushuhuda mzuri kuhusu mafanikio waliyoyapata," amesema Tutuba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa, Uhusiano na Masoko wa IAA, Sarah Goroi, amesema pamoja na chuo kuwa na mitaala inayokidhi mahitaji ya soko la ajira, pia kimeweka mkazo katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri kupitia Kituo cha Kuatamia Biashara cha IAA.

Amesema kituo hicho huwasaidia wanafunzi wenye vipaji na mawazo ya biashara kuyaendeleza hadi kuwa biashara halisi.

"Anapokuja mwanafunzi mwenye wazo au kipaji cha biashara, tunaanza kukiendeleza. Kufikia anapohitimu masomo yake anaweza kuwa tayari ana biashara au bidhaa iliyokomaa. Baada ya kuhitimu tunaendelea kumrasimisha ili aweze kuingia rasmi kwenye dunia ya biashara," amesema Goroi.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa masomo uliopita, kituo hicho kiliwafikia zaidi ya vijana 8,600, ambapo vijana 1,520 walibuni mawazo mbalimbali ya biashara na kufanikiwa kuanzisha zaidi ya biashara 50. Kati ya hizo, kampuni 11 zilisajiliwa rasmi.

Goroi amefafanua kuwa kampuni hizo zimejikita katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, teknolojia, sanaa, uhifadhi wa mazingira na maeneo mengine ya ubunifu, hatua ambayo imewawezesha wahitimu kujiajiri na pia kuajiri vijana wengine.

Amesema IAA itaendelea kuimarisha usimamizi wa Kituo cha Kuatamia Biashara, kilichozinduliwa mwaka 2020, ili kiendelee kuwa kitovu cha kukuza ubunifu, ujasiriamali na ajira kwa vijana nchini.

Post a Comment

0 Comments

USHIRIKIANO UMEONGEZA UFANISI WA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA