Na Judith Meingarai
KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kupitia uchunguzi wa kitaalamu wa sampuli, matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na utoaji wa ushahidi wa kisayansi unaosaidia kuimarisha ushindi wa kesi mahakamani.
Akizungumza wakati alipotembelea banda la GCLA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Kamishna Jenerali Lyimo alisema ushirikiano kati ya DCEA na GCLA umeendelea kuimarika na kuwa nguzo muhimu katika kutekeleza majukumu ya taasisi hizo kwa ufanisi.
Alisema sampuli zote zinazowasilishwa GCLA kwa ajili ya uchunguzi hupimwa kwa wakati na kwa usahihi, jambo linalowezesha wataalamu wa Mamlaka hiyo kutoa ushahidi wenye weledi mahakamani na hivyo kuongeza kiwango cha mafanikio katika kesi zinazohusu dawa za kulevya.
"Ushirikiano wetu na GCLA ni wa mfano. Majibu ya uchunguzi tunayapata kwa wakati pamoja na ushahidi wa kitaalamu unaotolewa na Wakemia mahakamani umechangia kwa kiwango kikubwa kushinda kesi mbalimbali zinazohusu dawa za kulevya," alisema Lyimo.
Aidha, aliipongeza GCLA kwa kuendelea kuwekeza katika vifaa na teknolojia za kisasa zinazowezesha kubaini aina mbalimbali za dawa za kulevya na kemikali husika, akieleza kuwa uwezo huo umeifanya Tanzania kuwa na mfumo imara wa uchunguzi wa kisayansi unaokidhi mahitaji ya sasa.
Alibainisha kuwa duniani kuna zaidi ya aina 1,430 za dawa za kulevya na kwamba uwezo wa GCLA wa kuzitambua na kuzichunguza kwa usahihi ni mchango mkubwa katika kuimarisha utekelezaji wa sheria na utoaji wa haki.
Kamishna Jenerali Lyimo pia aliwataka wafanyabiashara na wananchi kuhakikisha wanajiridhisha kuhusu kemikali zilizomo kwenye bidhaa wanazoingiza au kuuza nchini kwa kushirikiana na GCLA, pamoja na taasisi nyingine za udhibiti, ili kuepuka kujikuta wakikiuka sheria bila kufahamu.
"Baadhi ya wafanyabiashara wamejikuta wakikamatwa kwa kuuza bidhaa walizodhani ni salama, lakini baadaye kubainika kuwa zina kemikali zinazohusiana na dawa za kulevya. Ni muhimu kupata ushauri na uhakiki wa kitaalamu kabla ya kuingiza au kusambaza bidhaa hizo," alisisitiza.
Wakati huo huo, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la GCLA, Pasehsi Anthony mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, alisema elimu aliyoipata imemsaidia kuelewa kwa undani mchango wa Mamlaka hiyo katika mfumo wa haki jinai nchini.
Alisema kabla ya kutembelea banda hilo hakuwa akifahamu kuwa dawa zote za kulevya zinazokamatwa nchini lazima zipitie uchunguzi wa kisayansi katika maabara za GCLA ili kuthibitisha aina ya dawa husika kabla ya ushahidi huo kutumika mahakamani.
"Leo nimegundua kuwa GCLA ina jukumu kubwa zaidi kuliko nilivyokuwa nikifahamu. Uchunguzi wake wa kisayansi unasaidia kuthibitisha ukweli mahakamani na kuhakikisha haki inatendeka. Nawahamasisha wananchi wote watembelee banda hili ili wapate elimu muhimu kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hii," alisema Anthony.
Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Sabasaba, GCLA inaendelea kutumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake mbalimbali, ikiwemo uchunguzi wa kisayansi wa dawa za kulevya, kemikali, bidhaa, mazingira na vielelezo vya jinai, sambamba na kuhamasisha matumizi salama ya kemikali kwa maendeleo na usalama wa taifa.

0 Comments