EWURA YATOA WITO WA MATUMIZI SALAMA YA UMEME NA GESI YA LPG NANENANE


Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imewataka wananchi kuhakikisha wanafuata kanuni za usalama katika matumizi ya umeme na gesi ya mafuta ya petroli (LPG), ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha hasara za maisha na mali.

Akizungumza leo, Agosti 7,2026 katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo yanayoendelea katika Viwanja vya Dk.John Malecela, Nzuguni jijini hapa, Meneja wa EWURA Kanda ya Kati, Hawa Lweno, amesema wananchi wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya matumizi yasiyo salama ya mifumo ya umeme na gesi kutokana na kukosa elimu ya kutosha.

Amesema ni muhimu kuhakikisha kazi zote za ufungaji wa nyaya za umeme (wiring) zinafanywa na mafundi wenye sifa na wanaotambuliwa, kwani kufanya kazi hizo bila utaalamu kunaweza kusababisha hitilafu za umeme, moto na madhara mengine makubwa.

"Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu matumizi salama ya umeme na gesi ya LPG ili kulinda maisha yao na mali zao," amesema Lweno.

Ameongeza kuwa watumiaji wa gesi wanapaswa kuhakikisha mitungi na vifaa vinavyotumika vimekaguliwa na vinakidhi viwango vya usalama, pamoja na kuzingatia maelekezo yote ya matumizi ili kupunguza hatari za ajali.

Lweno ameeleza kuwa EWURA inaendelea kutumia maonesho ya Nanenane na majukwaa mengine ya umma kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya nishati, pamoja na kuwahamasisha kutumia huduma zinazokidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka hiyo.

Aidha, amewahimiza wananchi kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu wanapokutana na changamoto za mifumo ya umeme au gesi badala ya kufanya marekebisho wenyewe, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha usalama wa familia na jamii kwa ujumla.

Amesema EWURA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu ya matumizi salama ya nishati inawafikia wananchi wengi zaidi ili kujenga jamii inayotumia nishati kwa ufanisi na usalama.

Post a Comment

0 Comments

FCC YAIMARISHA ELIMU YA USHINDANI NA ULINZI WA WALAJI