Na Asha Mwakyonde, DODOMA
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewataka wanafunzi waliomaliza kidato cha sita pamoja na wenye diploma kutumia mfumo wa udahili wa mtandaoni (OAS), kuwasilisha maombi ya kujiunga na chuo hicho kwa mwaka wa masomo husika.
Akizungumza leo Agosti 8 2026,katika banda la UDOM kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane jijini Dodoma, Afisa Udahili kutoka chuo hicho, Shikunzi Mwashusa amesema UDOM imeweka huduma ya kuwasaidia waombaji wanaohitaji kufanya maombi ya udahili kwa ngazi ya diploma na shahada.
Amesema mwombaji anapaswa kuanza kwa kutengeneza akaunti katika mfumo wa OAS kwa kutumia namba yake ya mtihani wa kidato cha nne na kuweka nenosiri atakalotumia kuingia katika mfumo.
Amefafanua kuwa baada ya kuingia, mwombaji anatakiwa kujaza taarifa zake binafsi kwa usahihi, kisha mfumo utampeleka kwenye hatua ya malipo na kumpatia namba ya malipo (control number).
Mwashusa amesema baada ya kufanya malipo, mwombaji ataweza kuendelea na hatua ya kuchagua programu za masomo, ambapo mfumo utaonyesha programu anazostahili kuomba kulingana na sifa zake.
“Baada ya kuweka machaguo yake, mwombaji atapata nafasi ya kuya-preview na kujiridhisha kama amefanya uchaguzi sahihi, kisha atathibitisha na kutuma maombi yake kwa Chuo Kikuu cha Dodoma,” amesema.
Amesema mwombaji anapaswa kuweka jumla ya machaguo matatu ya programu, kwa kuzingatia zile anazokidhi vigezo vya udahili.
Aidha, amesema awamu ya kwanza ya udahili UDOM inatarajiwa kufungwa Agosti 10, hivyo amewataka waombaji ambao bado hawajakamilisha maombi kutumia muda uliobaki kuwasilisha maombi yao.
Mwashusa ameongeza kuwa baada ya kufungwa kwa awamu hiyo, chuo kitaanza mchakato wa kuchakata maombi kwa ajili ya kuwatambua na kuwaandaa waombaji watakaopata nafasi ya kujiunga na UDOM.

0 Comments