Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MVUA kubwa zinazotarajiwa kunyesha kutokana na hali ya El Niño zimeisababisha Serikali kuongeza kasi ya maandalizi ya kukabiliana na mafuriko, maporomoko ya ardhi, milipuko ya magonjwa na madhara mengine yanayoweza kuathiri maisha ya wananchi, uchumi na miundombinu nchini ambapo inakadiriwa kuhitaji rasilimali za takribani shilingi bilioni 730 kutekeleza shughuli mbalimbali za maandalizi, kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa.
Akizungumza leo Septemba 2, 2026 jijini hapa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Niño, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kiasi hicho ni makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutoka kwa Serikali na wadau mbalimbali, na si fedha zote zilizotengwa moja kwa moja na Serikali kwa ajili ya El Niño.
Prof. Kabudi amesema katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027, shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo kwa sekta zote, huku shughuli nyingine zikiendelea kutekelezwa na wizara, taasisi na wadau mbalimbali kupitia bajeti zao.
Ameeleza kuwa mpango huo umeandaliwa kufuatia utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wa Agosti 18, 2026, ulioonesha uwepo wa El Niño yenye nguvu, inayoweza kusababisha mvua kubwa, mafuriko, maporomoko ya ardhi, milipuko ya magonjwa kwa binadamu na wanyama pamoja na uharibifu wa miundombinu na mali.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, mpango huo umeandaliwa kwa ushirikishwaji wa wizara, idara na taasisi za Serikali, mikoa na halmashauri, mashirika ya kitaifa na kimataifa, Umoja wa Mataifa, asasi zisizo za kiserikali, sekta binafsi na wadau wengine.
Amefafanua kuwa shughuli zitakazotekelezwa zinahusisha ukarabati na uboreshaji wa barabara, madaraja, reli, makaravati na mitaro, pamoja na kuimarisha miundombinu ya afya, elimu, maji, umeme, mawasiliano na huduma nyingine muhimu katika maeneo hatarishi.
Aidha, amesema Serikali imepanga kuimarisha akiba ya chakula, kuweka vifaa vya uokoaji na misaada ya kibinadamu katika maghala ya kikanda, kutenga maeneo salama kwa ajili ya makazi ya muda na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na madhara ya mafuriko, radi, maporomoko ya ardhi na magonjwa ya mlipuko.
Prof. Kabudi pia amewataka wananchi kutumia fursa ya mvua hizo kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi na uvunaji wa maji, huku wakichukua tahadhari kwa kufanya shughuli zao katika maeneo salama.
"Maeneo yote hatarishi yanapaswa kutambuliwa mapema, kufanyiwa tathmini ya vihatarishi na wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuhamasishwa kuhamia maeneo salama endapo kutakuwa na tishio la maafa," amesema.
Aidha, amezitaka wizara, taasisi, mikoa na halmashauri kufanya ukaguzi wa miundombinu muhimu na kuhakikisha madaraja, makaravati na mitaro inaimarishwa na kusafishwa ili huduma muhimu ziendelee kupatikana wakati wote.
Prof. Kabudi amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuchukua hatua kwa wakati, huku akiwataka wadau na vyombo vya habari kutoa taarifa sahihi ili kuondoa taharuki kuhusu maandalizi ya kukabiliana na El Niño.
“Usimamizi wa maafa ni jukumu letu sote, shiriki sasa na chukua hatua,” amesema Prof. Kabudi.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu tayari imewaelekeza Wakuu wa Mikoa inayotarajiwa kuathiriwa na mvua hizo kuchukua hatua za maandalizi na kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza.



0 Comments