Dar es Salaam
UELEWA wa wananchi kuhusu hifadhi ya jamii na uwekezaji unatarajiwa kuimarika baada ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) kuanzisha ushirikiano wa kimkakati unaolenga kutumia nguvu ya vyombo vya habari vya mtandaoni kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Ushirikiano huo umeibuliwa wakati timu ya maofisa waandamizi kutoka PSSSF ilipofanya ziara katika makao makuu ya muda ya TBN, Kijitonyama, Dar es Salaam, ambapo pande hizo zilifanya mazungumzo kuhusu namna ya kuimarisha utoaji wa taarifa sahihi kuhusu hifadhi ya jamii, pensheni na uwekezaji.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo uko tayari kushirikiana na PSSSF katika kutoa elimu kwa umma, akisisitiza umuhimu wa wanachama wa TBN kupewa mafunzo ya kina kuhusu shughuli na huduma zinazotolewa na mfuko huo.
Alisema baada ya kupata uelewa wa kutosha, wanablogu na waandishi wa mtandao watakuwa katika nafasi nzuri ya kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na zinazoeleweka kuhusu hifadhi ya jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo inalenga kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa habari huku akisisitiza umuhimu wa kutumia majukwaa ya kidijitali katika kuongeza uelewa wa wananchi.
Njaidi alisema hoja na mapendekezo yaliyowasilishwa na TBN yatafanyiwa kazi, akieleza kuwa ushirikiano huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu masuala ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na PSSSF.
Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo unaendelea kutumia weledi na majukwaa ya kidijitali kuhakikisha Tanzania inaendelea kusomeka vizuri katika ulimwengu wa kidijitali na kuchochea maendeleo.
Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo uko tayari kutumia waandishi wake na majukwaa mbalimbali kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na za kuaminika kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii.
Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa zaidi kwa vyombo vya habari vya mtandaoni kushiriki katika kutoa elimu kwa umma na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandaa kwa maisha ya baada ya ajira kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii.
Katika mkutano huo, ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kujumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo.
Kwa upande wa TBN, viongozi walioshiriki ni Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano Cathbert Kajuna pamoja na Mdhamini wa mtandao huo, Issa Michuzi.



0 Comments