SELF MF, WODESU WAFUNGUA FURSA ZA MITAJI KWA WANAWAKE 1,450 DODOMA

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

WANAWAKE wajasiriamali 1,450 jijini Dodoma wamefikiwa na huduma za mikopo zinazolenga kuimarisha mitaji yao na kukuza biashara, kupitia ushirikiano kati ya Self Microfinance Fund (SELF MF) na Wodesu Microcredit, unaowapa nafasi zaidi wafanyabiashara wadogo kupata huduma za kifedha, wakiwemo wauzaji wa mboga za majani ambao hukabiliwa na changamoto ya kupata mikopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wodesu Microcredit, Melina Faustine, ameyasema hayo leo Oktoba 15,2026 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya SELF MF katika taasisi hiyo jijini hapa amesema ushirikiano  huo umeongeza uwezo wa taasisi yake kuwafikia wanawake wengi zaidi wanaohitaji mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara, kuongeza mtaji na kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Ameeleza kuwa mikopo hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kuwafikia wanawake ambao wamekuwa na changamoto ya kupata huduma za kifedha katika baadhi ya taasisi za mikopo.

“Kupitia mikopo ya SELF MF nimeweza kuwafikia wanawake 1,450, wakiwemo wale wanaouza mboga za majani ambao si rahisi kupata mikopo katika sehemu nyingine,” amesema.

Hata hivyo, Faustine ameeleza kuwa baadhi ya waombaji wamekuwa wakiwasilisha taarifa za biashara ambazo si zao wakati wa kuomba mikopo, akionya kuwa hali hiyo inaweza kusababisha fedha kutotumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuathiri urejeshaji wa mikopo kwa wakati.

Amesema utoaji wa taarifa sahihi ni muhimu katika kuhakikisha mikopo inawafikia walengwa wanaostahili, huku marejesho ya wakati yakisaidia kuendeleza mzunguko wa fedha na kuwezesha wajasiriamali wengine kunufaika na fursa hizo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya SELF MF, Paul Sangawa, amesema ziara hiyo imelenga kujionea namna mfuko huo unavyoshirikiana na taasisi za kifedha katika kuwafikishia wananchi huduma za mikopo na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Amesema taasisi kama Wodesu Microcredit zina nafasi muhimu katika kusogeza huduma za kifedha karibu na wafanyabiashara wadogo, hususan wanawake wanaohitaji mitaji ya kuanzisha, kuimarisha na kupanua biashara zao.

Sangawa amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa matumizi ya mikopo na marejesho yake ili kuhakikisha fedha hizo zinaendelea kuwafikia wananchi wengine wenye mahitaji ya mitaji.

“Wananchi wengi wana mahitaji ya mikopo na hii ni mojawapo ya fursa wanazoweza kuzitumia kujikwamua kiuchumi na kuanzisha shughuli mbalimbali zinazoweza kuwasaidia kuboresha maisha yao,” amesema.

Naye Msemaji Mkuu wa SELF MF, Santieli Yona, amesema mfuko huo una aina mbalimbali za mikopo zinazolenga kukidhi mahitaji ya makundi tofauti ya wananchi, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na wafanyakazi wa Serikali, pamoja na kusaidia taasisi za kifedha kupanua huduma za mikopo.

Amesema SELF MF hutoa mikopo kwa taasisi za kifedha zilizosajiliwa kisheria, vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), pamoja na mikopo ya moja kwa moja kwa watu binafsi, kwa kuzingatia aina ya huduma na vigezo vilivyowekwa.

Yona amewahimiza Watanzania kutumia fursa hizo kwa kuwasilisha maombi yanayokidhi vigezo, kuelewa masharti ya mikopo na kuwa na mipango madhubuti ya biashara itakayowawezesha kutumia mitaji kwa tija.

“Tunakaribisha Watanzania wote waje SELF MF kwa sababu tuna mikopo ya aina mbalimbali kwa ajili ya biashara na shughuli tofauti za kiuchumi. Lengo letu ni kuwawezesha wananchi kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao,” amesema.

Amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya mikopo, usimamizi mzuri wa fedha na urejeshaji kwa wakati ni mambo muhimu katika kukuza biashara, kuongeza kipato na kuhakikisha fursa za mikopo zinaendelea kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.


 

Post a Comment

0 Comments

MMUYA ATOA KONGOLE KWA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI MSUMBIJI KWA KUENDELEA KUIMARISHA DIPLOMASIA YA UCHUMI