Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
HISTORIA ya ushiriki wa wanawake katika ulinzi na usalama imeendelea kuandikwa kupitia mafanikio ya Meja Jenerali Mstaafu Zawadi Madawili, mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki kufikia cheo cha Meja Jenerali, ambaye mchango wake katika utumishi wa kijeshi umetambuliwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt. Rhimo Nyansaho.
Dkt. Nyansaho alifanya ziara ya kumtembelea Meja Jenerali Mstaafu Madawili Novemba 16, 2026, katika makazi yake yaliyopo Upanga, jijini Dar es Salaam, ambapo walipata fursa ya kuzungumzia safari yake ya utumishi wa kijeshi, mafanikio na mchango wake katika kulinda na kuitumikia nchi.
Mazungumzo hayo pia yalilenga kumjulia hali kiongozi huyo mstaafu na kubadilishana uzoefu kuhusu safari yake ya uongozi ndani ya Jeshi, pamoja na hatua mbalimbali alizopitia hadi kufikia cheo cha Meja Jenerali.
Meja Jenerali Mstaafu Madawili ana nafasi ya kipekee katika historia ya ulinzi na usalama Afrika Mashariki, kutokana na kuwa mwanamke wa kwanza kufikia cheo hicho, mafanikio yanayoonesha nafasi na uwezo wa wanawake katika utumishi wa kijeshi.
Ziara hiyo imekuwa sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wake katika historia ya Jeshi, huku safari yake ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake wanaotamani kushiriki katika utumishi wa kijeshi na kushika nafasi za uongozi.

0 Comments