TANZANIA INAHITAJI ALAMA YA BIASHARA YA KIPEKEE KUTAMBULISHA BIDHAA ZA KILIMO NJE YA NCHI- BASHE


 NA MWANDISHI MAALUMU

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe(Mb) amesema imefika wakati  sasa  kwa Taasisi zinazohusika na masuala ya Miliki Ubunifu kuja na mapendekezo yatakayowezesha Tanzania kuwa na alama ya biashara ya kipekee itakayotambulisha  bidhaa za Tanzania duniani kote.

Waziri Bashe ametoa rai hiyo   tarehe 02 Novemba, 2022 jijini Dodoma alipotembelewa ofisini kwake  na ujumbe kutoka  Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO) ambalo makao makuu yake yako  Harare- Zimbabwe, ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shrikika hilo Bw. Bemanya Twebaze, aliyeambatana na Mwenyeji wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa.

Mhe. Bashe amesema Tanzania ikiwa na alama yake ya biashara ya kipekee mfano  kwa bidhaa zake zote za kilimo zinazouzwa nje ya nchi itawezesha kutambulika duniani kote na thamani ya bidhaa hizo kuongezeka tofauti na ilivyo sasa ambapo bidhaa nyingi zinauzwa nje ya nchi lakini hazitambuliki kama bidhaa za Tanzania kama nchi. Pia kutumika kwa Alama ya Tanzania kutazitangaza bidhaa za kilimo kutoka Tanzania. Hii itasaidia kujua mnyororo wa thamani wa bidhaa zote za kilimo.

“Ukiangalia bidhaa ya Champagne ni mvinyo unajulikana duniani kote kutokana  jina la mahali bidhaa hiyo ilikozalishwa kwa mara ya kwanza nchini Ufaransa, Ifike wakati sasa bidhaa za Tanzania zijulikane kwa alama ya kipekee duniani kote”, amesisitiza Mhe. Bashe.

Akizungumzia  Ufadhili wa wanafunzi watano kila mwaka  wanaosomea Shahada ya Uzamili ya Masuala ya Miliki Ubunifu  katika Chuo Kikuu cha Dar  es Salaam chini ya ufadhili wa BRELA, wakati ARIPO  ikitoa utaalam wa kiufundi na ufadhili, ameshauri pia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC) pia zijumuishwe kwenye mpango huo kwani vumbuzi nyingi zinafanyika katika taasisi hizo hivyo ni vyema zikawezeshwa zaidi.

Mhe. Bashe amesema katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na ARIPO za kuendeleza Miliki Ubunifu kwa nchi wananchama wa ARIPO wizara yake itaridhia Itifaki ya Arusha inayohusu ubunifu wa aina mpya ya mbegu za mimea iliyosainiwa Arusha mwaka 2015 na kuelekeza  viongozi wa Wizara ya Kilimo kuanza  mchakato wa kuridhiwa kwa Itifaki ya Arusha, kwani haileti picha nzuri kwa kutoridhia Itifaki iliyosainiwa mwaka 2015 Mkoani Arusha.

Awali  akimtambulisha Bw, Twebaze, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw, Nyaisa amesema BRELA ikiwa ni miongoni mwa wanachama wa ARIPO imekuwa ikinufaika na mafunzo mbalimbali  yanayotolewa  na Shirika hilo  ya kuwajengea uwezo watumishi wa BRELA.
Bw. Nyaisa amesema BRELA inatambua umuhimu wa Miliki Ubunifu  kwa Tanzania ndiyo maana imekuwa mstari wa mbele kutoa ufadhali  wa masomo kwa Watanzania ili wawe chachu katika kuhakikisha kuwa wabunifu wananufaika na bunifu zao  na kulindwa kisheria.

Kwa upande wake Bw, Twebaze ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano  ambao ARIPO inaupata kupitia BRELA kwani  ujumbe huu ukiwa nchini Tanzania umekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya Umma zinazojihusisha na masuala ya Ubunifu wa aina mpya ya  mbegu za mimea chini ya Itifaki ya Arusha ambayo  inasubiri kuridhiwa.

Ameeleza  pia baada ya kufanya ziara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuzungumza na uongozi wa chuo hicho  ameridhishwa na mashirikiano yaliyopo kati ya Chuo Kikuu  cha Dar es Salaam na 
BRELA katika kufanikisha ufadhili wa masomo ya Shahada ya Uzamili kwa wanafunzi ambao wanatoka nchi wanachama wa ARIPO ikiwemo Tanzania. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uwekezaj, Viwanda na Biashara Mhe, Exaud Kigahe (Mb) alipokutana na ujumbe huo wa ARIPO katika ofisi za BRELA jijini Dodoma, ameahidi wizara yake kufuatilia kwa karibu ili Itifaki ya Arusha  iridhiwe mapema na kuanza kutumika ambayo itawezesha upatikanaji wa mbegu na  uzalishaji wa chakula cha kutosha kutokana na ubunifu wa aina mpya ya mbegu za mimea.

“Itifaki hii ni muhimu na itaridhiwa   mapema iwezekanavyo  kwani nchi inahitaji kujitosheleza  kwa chakula hivyo ni vyema  bunifu hizi zikalindwa  ikiwa ni pamoja na wahusika kunufaika”, amesisitiza Mhe, Kigahe.

Ujumbe wa ARIPO ambao umeondoka leo tarehe 3 Novemba, 2022 kurejea nchini Zimbabwe umekuwepo nchini kwa siku nne na mbali ya kukutana na viongozi pamoja na wadau, pia ulipata fursa ya kutembelea mji wa Serikali wa Magufuli uliopo Mtumba jijini Dodoma, pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa ambapo  Bw. Twebaze amepongeza maendeleo yanayofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungazo wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Imeandaliwa na Kitengo  Habari-BRELA

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU