UHABA WA MAJI UNAVYOWATESA WAKAZI WA KIJIJJ CHA DAKI,WILAYANI CHEMBA


Na Asha Mwakyonde, Chemba

WAKAZI wa kijiji cha  Daki kilichopo Kata ya Mondo Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wameiomba serikali kuharakisha umeme ili waondokane na adha ya maji safi na salama ambapo kwa sasa wanatumia ya  kisima kilichochimbwa na Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA),ambacho kinatumia Sola.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao wakazi wa kijiji hicho wamesema kuwa wanatumia muda mwingi kusubiri foleni ya kuteka maji ya kisima kilichochimbwa RUWASA,jambo ambalo linakwamisha shughuli zao nyingine za kimaendeleo.

Rukia Mkuyu ni mkazi wa kijiji hicho Cha Daki ameeleza kuwa wanakabiliwa na changamoto ya maji ambapo  wanaweka foleni ya kusubiri kuteka maji kuanzia asubuhi hadi saa tisa alasiri.  

Ameongeza kuwa kutokana na tatizo la maji walilonalo wanalazimika kupeleka ndoo zao usiku au kuweka alama ili kesho yake wapate maji na wakati mwingi yanaweza kutoka saa moja tu na kukatika inategemea na hali ya hewa.

Rukia amesema kuwa mtu asipoweka alama au ndoo tangu jana yake  anaweza kwenda bombani hapo asubuhi na asipate maji hadi jioni.

Naye Mwajuma Mwenda (67), ameiomba serikali kuharakisha kupeleka umeme katika kijiji hicho ili waweze kuondokana na tatizo la maji kwa kuwa wanatumia muda mwingi kwenye maji kuliko kufanya shughuli nyingine muhimu. 

"Tungu nimefika hapa saa tano ya asubuhi hadi muda huu ni saa 11 jioni  ninavyoongea na wewe ndio napata maji, maji haya yanatumia sola siku kukiwa na wingu tunakosa maji,"ameeleza Mwajuma.

Ameongeza kuwa kukiwa na wingu kubwa wanaenda kuteka maji msikitini  na kwamba wanaenda kulundikana hapo na inapofika muda wa ibada wanapisha kwa muda halafu wanarudi tena.

UONGOZI WA KIJIJJ

Akizungumzia kero hiyo ya maji mwenyekiti wa kijiji cha Daki,Bunge Tesa amesema kijiji hicho ni kikubwa wanakabiliwa  na changamoto mbalimbali  ikiwamo tatizo la maji ambapo wanakisima ambacho kinatumia Sola.


Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa katika kisima hicho tayari zimechimbiwa nguzo mbili za kuwekwa transifoma lakini  tangu zichimbiwe hadi sasa hazijashughulikiwa tena hivyo  jua lisipowaka vizuri maji hayatoki hali inayosababisha wananchi kupata adha hasa wanawake.

Ameongeza kuwa kijiji hicho kina wakazi wengi na hawajapata umeme huku akisema nguzo za umeme  zilizofikishwa kijikini hapo ni 22.

Tesa amefafanua kuwa akina mama wanapoenda kuteka maji wanaangalia hali ya hewa kama jua halijawaka vizri wanachota ndoo mbili mbili ili wapate maji wote wenye zamu yao na waliowahi kuweka foleni tangu jana yake.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU