Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Kulia) akimkaribisha Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Philipo Gekul (kushoto) alipowasili katika ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Katiba na Sheria mapema leo Tarehe 28/02/2023.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Philipo Gekul akipokea taji la maua mara baada ya kuwasili katika ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Philipo Gekul pamoja na wajumbe wa menejimenti na watumishi wakiwa katika picha ya pamoja. Na Lusajo Mwakabuku – WKS
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Philipo Gekul amewasili katika ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Katiba na Sheria na kulakiwa na umati wa Viongozi, Menejimenti na Watumishi wa Wizara hiyo akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro mapema leo Tarehe 28/02/2023 mara baada ya kuapishwa jana jioni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu ya Chamwino – Dodoma.
Akitoa salamu za ukaribisho baada ya utambulisho mfupi wa watumishi waliokuwepo ofisini, Mhe. Damas Ndumbaro akiwa ofisini kwake alimwambia Naibu Waziri mpya kuwa Wizara inamkaribisha na ipo tayari kuhakikisha kuwa inampa ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha kuwa anatekeleza majukumu yake ipasavyo bila vikwazo vyovyote.
Aidha Mhe. Ndumbaro aligusia suala lililoongelewa na Mhe. Rais juu ya uamuzi wake wa kuwabadilisha Mawaziri na Makatibu Wakuu kuwa umetokana na badhi ya viongozi hao kutokuwa na maelewano. Ndumbaro amesema kuwa moja ya sababu zinazosababisha viongozi kutokuwa na amani na upendo ni kukosekana kwa mawasiliano mazuri kati yao yanayopelekea kukosekana kwa ufanyaji kazi wa pamoja (teamwork). Kukosekana kwa ufanyaji kazi wa pamoja kunapelekeana viongozi kufikiriana vibaya na hivyo kupelekea misuguano isiyo na tija kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wa Mawaziri na Manaibu wao, Ndumbaro alisema ugomvi mkubwa huwa unatokana na Manaibu Mawaziri kutopewa majukumu na hivyo akaanza kwa kumuagiza kuwa pamoja na majukumu mengine atakayompangia, masuala yote ya Bunge litakuwa ni jukumu la Mhe. Naibu Waziri Gekul. Aidha Mhe. Ndumbaro akamtaka Mhe. Gekul kuhakikisha anatumia muda wa kutosha kuweza kuifahamu Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake kwa upana wake kwani ina taasisi kubwa ikiwemo muhimili wa Mahakama ili aweze kufahamu mipaka yake katika kuiongoza Wizara.
Akitoa shukrani zake baada ya mapokezi hayo, Mhe. Naibu Waziri Gekul alianza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumpa nafasi katika kuendelea kuitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia akawaomba watumishi wote wa Wizara kumpokea katika familia ya Katiba na Sheria na kumpa ushirikiano katika kuhakikisha anatekeleza yale ambayo Rais amemtuma kuyafanya pamoja maelekezo atakayoagizwa na Waziri wa Katiba na Sheria.
0 Comments