Na Asha Mwakyonde, Dodoma
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ( NEMC) limesema limepokea malalamiko 369 ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira kutoka kwa wananchi ikiwemo kelele za muziki katika Mabar pamoja na kushamiri kwa gereji bubu.
Pia NEMC yajuvunia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia michakato mingi ya mabadiliko ikiwemo katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki akiwa Makamu wa Rais wa awamu ya tano.
Hayo yameelezwa Machi 3,2023 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC,Dk.Samweli Gwamaka wakati akielezea mafanikio ya Baraza hilo katika kipindi ya miaka miwili ya utawala wa Serikali ya awamu ya Sita kwa waandishi wa habari ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazojivunia kukomesha matumizi ya mifuko ya plastiki
Akizungumzia mafanikio mengine Dk. Gwamaka amesema ni pamoja na kuanzisha sera mpya ya mazingira ya mwaka 2021na kuseman kuwa sera iliyokuwepo ambayo ilitungwa mwaka 1997 pamoja na uzuri wake haikuendana na Muda.
Dk. Gwamaka ameongeza kuwa mazingira na kasi ya maendeleo, madiliko ya sayansi na Teknolojia, wameboresha upatikanaji wa huduma zao kwa wateja wao ambapo kwa sasa huduma ni saa 24.
Amesema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa ofisi za Kanda Kutoka 5-13,Uteuzi wa wakaguzi wa mazingira 405,Kuongezeka Kwa mapato yaliyowezesha NEMC kuchangia kiasi Cha shilingi bilioni 9 Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita,Upandaji wa miti maeneo mbali mbali ya nchi pamoja na utoaji wa vibali.
"Tuna changamoto kadhaa na katika kukabiliana nazo ,tunayo mipango mbali mbali ikiwemo ya kuwekeza katika kutoa elimu ya mazingira na uhifadhi wa mazingira kwa wananchi,Uanzishaji wa klabu za mazingira kwa shule za msingi na sekondari," amesema Dk.Gwamaka.
Aidha amewataka wananchi kuunga mkono katika mipango na Utii wa sheria na kanuni mbali mbali za uhifadhi,utunzaji na ustawishaji wa mazingira na kwamba baraza hilo halitasita kuchukua hatua kali za kisheria atakayekiuka sheria,taratibu na kanuni zilizowekwa.
0 Comments