WCF IMEONGEZA KIMA CHA CHINI CHA FIDIA HADI KUFIKIA 275,333.


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

SERIKALI kupitia  Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), imetekeleza Sera ya kuongeza kima cha chini cha fidia hadi kufikia Shilingi 275,333 kutoka utaratibu wa awali ambao haukuwa na kima cha chini cha fidia kwa mfanyakazi ambaye hakupata ulemavu wa asilimia 100 .

Akizungumza jijini Dodoma Machi 02,2023 kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2023,Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dk.John Mduma  amesema kuwa mfuko huo ulifanyiwa tathmimi ya uhai na uhimilivu mwaka 2018 na kuonekana kwamba ipo imara hadi mwaka 2047.

Dk. Mduma ameeleza kuwa mwaka huu wameshaanza mchakato wa kufanyiwa tathmini nyingine, tunaamini kwa utekelezaji  walionao WCF ni imara kwa zaidi ya miaka mingine 30 ijayo.


"Nawaomba waajiri wote nchini kuendelea kutekeleza wajibu wao kwenye Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Mwajiri ndiye mwenye jukumu la kuchangia kwenye Mfuko wa WCF na ni kosa la jinai kutofanya hivyo," amesema Mkurugenzi huyo.

Akizungumzia kuhusu kusajili Waajiri Tanzania Bara amesema hadi kufikia June 30 mwaka jana WCF imesajili jumla ya waajiri 27,786 ikiwa ni asilimia 90 ya waajiri 30,846 walioko kwenye kanzidata ya Mfuko na kufikia mwezi Februari 2023 imesajili jumla ya waajiri 29,978 na kwamba kutoka Machi 2021 hadi Februari 2023,ilisajili jumla ya waajiri 5,250.

Dk. Mduma ameongeza kuwa waajiri wakubwa wanachangia kiasi kinachozidi Shilingi Milioni 1.5 kwa mwezi, waajiri wa kati wanaochangia kati ya Shilingi 250,000 na Shilingi Milioni 1.5 kwa mwezi na waajiri wadogo
wanachangia chini ya Shilingi 250,000 kwa mwezi.

Amefafanua kuwa Mfuko huo  ulianza rasmi kukusanya michango kwa Waajiri kuanzia  Julai1,2015 hadi kufikia Juni 30 2022, makusanyo ya jumla ya michango yalifikia Shilingi Bilioni 545.49.

"Shilingi Bilioni 88.07 zilikusanywa mwaka wa fedha 2020/2021 na Shilingi Bilioni 86.65 zilikusanywa mwaka wa fedha 2021/2022 na hadi kufiki Juni 30 2022, Mfuko umekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 241.48 toka kwenye mapato yatokanayo na uwekezaji," ameeleza.

Ameongeza kuwa WCF ilitengeneza Shilingi Bilioni 69.86 katika mwaka wa fedha 2020/2021 na Shilingi Bilioni 74.29 katika mwaka wa fedha 2021/2022 na kwamba jumla ya mali za Mfuko hadi 30 Juni 2022 ni Shilingi Bilioni 545.16.


Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU