MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA),imesema katika mwaka wa fedha 2022/23, imefanya uchambuzi wa sampuli 1,025 za viuatilifu ambapo sampuli 1,005 sawa na asilimia 98.04 zilikidhi viwango na sampuli 20 sawa na asilimia 1.96 hazikukidhi.
Akizungumza jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Dk.Joseph Ndunguru ameeleza kuwa Mamlaka hivyo imeendelea kufanya kaguzi za biashara ya Viuatilifu ili kupunguza uwepo wa viuatilifu bandia.
Pia Dk. Ndunguru amesema jumla ya viuatilifu vipya 409 na kampuni za ufukizaji 198 vimesajiiliwa na kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo, imefanya uchambuzi wa sampuli za udongo takribani 1,300 kutoka kwenye mashamba ya “Block farming” lengo likiwa ni kuwezesha biashara ya mazao.
"Sampuli 40 zilifanyiwa uchambuzi kwenye mazao mbalimbali na sampuli zote zilikidhi viwango na biashara ya mazao ilifanyika,TPHPA imeanza rasmi Julai, 2022 kwa ajili ya kukidhi matakwa ya masoko na mikataba ya kimataifa (IPPC) pamoja na Mazingira salama kwa Afya ya Binadamu, Wanyama na Mimea," amesema.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23, Mamlaka imeboresha maabara za kikemia na kibaiolojia na imefanikiwa kupata ithibati kwenye maabara ya uchambuzi wa viuatilifu (ISO 17025:2017)
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi huyo Mamlaka imeboresha mfumo wa utoaji huduma ambao ni mfumo rafiki kwa wadau, unawapunguzia wateja gharama za ziada, unatoa vibali kwa haraka, na unaonesha taarifa za ukusanyaji wa mapato ya Mamlaka.
0 Comments