Na Asha Mwakyonde,Dar es salaam
KAIMU Mkurugenzi Ofisi ya Afrika ya
Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF),
ambaye pia ni Mkurugenzi mkazi wa Ofisi ya shirika hilo nchini Tanzania Amani Ngusaru amesema serikali inaelewa na inajitahidi kuzungumzia mambo ya mazingira na kwamba imekuwa ikitilia mkazo suala la utunzaji wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam mara baada ya kumalizika kwa mkutano Zoom uliofanywa na baadhi ya nchi za afrika ameeleza kwa Rais Dk.Samia suluhu Hassan na Makamu wake Dk. Philip Mpango wanaposimama kuzungumza wanazungumzia mambo ya mazingira na kupanda miti.
Mkurugenzi huyo amesema wametambulisha kampeni mpya inayoitwa 'Toa dakika 60' (60 EARTH HOUR),kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira kwa mwaka na kwamba
katika siku hiyo hapa nchini imeleta mafanikio makubwa kwa kuwa wao kama WWF wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali katika jamii.
"Hii inatupa mwanya kwa jamii na mtu mmoja mmoja kuweza kushiriki kwa kutoa saa moja kwa mwaka," amesema.
Akizungumzia siku hiyo ameeleza kuwa kwa hapa nchini bado haina mwamuko mkubwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika ambapo shughuli zinasimama kwa saa moja kutambua umuhimu wake.
Ameongeza kuwa mwamko kwa serikali upo lakini kwa wananchi na mtu mmoja mmoja kutokana na madhila waliyonayo wanajisahau kuwa mabadiliko ya tabia nchi ndio namba moja bila kuheshimu mazingira hata kula kutakuwa kwa mashaka.
Mkurugenzi huyo amesema mabadiliko ya tabia nchi yanaanzia katika anga na kubadilisha mifumo na ndio tatizo linaanza la majanga ya asili ambapo mvua inanyesha kwenye kipindi ambacho mkulima hajui analima saa ngapi.
Amesema kuwa majanga ya asili yanaweza kusababisha tatizo la ukosefu wa chakula na kwamba mvua zinaponyesha katika kipindi ambacho mkulima hatarajii kulima na kwamba hiyo inatokana na kutotuzwa kwa vyanzo vya maji na mazingira ambapo mkulima huyo anaweza kulima kilimo cha kumwagiliaji.
Ngusaru akizungumzia hali ilivyo barani Afrika amesema takriban watu milioni 600 wanakosa huduma za msingi za upatikanaji wa nishati ya uhakika na safi huku zaidi ya watu bilioni moja katika nchi 54 wakikosa huduma ya kupozea ambayo ni muhimu kwa usalama wa chakula, vifaa tiba, maisha na kuzuia vifo vinavyotokana na joto.
"Afrika lazima pia ihifadhi rasilimali ili kuhakikisha ufikiaji wa nishati mbadala kwa kutumia jua kubwa la upepo, nishati ya maji na rasilimali za jotoardhi," amesema.
Awali Meneja Mawasiliano wa WWF, Ofisi ya Shirika hilo nchini Tanzania Joan Itanisa amesema kuwa mwaka huu wametambulisha kampeni hiyo lengo likiwa ni kuhamasisha jamii,vikundi vya uhifadhi mazingira angalau mara moja kwa mwaka watoe dakika zao 60 waache yale wanayoyafanya na kuweza kuwekeza katika uhifandhi wa mazingira.
Joan amesema Machi 25 watakuwa Pugu mnadani ambapo ni chanzo cha mto Msimbazi kwa ajili ya kufanya usafi na kupanda miti 5000 ndani ya wiki moja.
"Pia tunawahamasisha watu wengine ambao hawawezi kuungana na sisi kule kule walipo waweze kupanda miti,kutoa elimu ya uhifandhi wa mazingira, kufanya usafi katika dakika 60 za uhifandhi wa mazingira," amesema Joan.
0 Comments