WWF YAHAMASISHA JAMII KUTUMIA DAKIKA 60 'EARTH HOUR' KUPANDA MITI


 Na Asha Mwakyonde, Dar es salaam

KIWANGO cha maji ya kutiririka kwenye  mto Msimbazi kitaongezeka na maji yanayotiririka wakati wa kiangazi yatapungua ndani ya miaka miwili au mitatu endapo miti itapandwa  kutokana na mimea kubeba maji asilimia 80 hivyo upandaji miti ni muhimu ili kupata maji tiririka.

Mto Msimbazi kwa takribani siku 215 upo mkavu (Dry channel), na kwamba maji yakitiririka ndani ya siku hizo yatakuwa yanatoka katika makazi ya Watu yakiwamo maji taka kwa kuwa hapatakuwa na maji ya asili ndani siku hizo 215.

Hayo yamesemwa jijini  Dar es salaam Machi 25,2023 na Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Shaban Yusuf wakati wa upandaji miti katika bonde la mto Msimbazi ikiwa ni maadhimisho ya siku ya uhifadhi wa Mazingira duniani ambayo huadhimishwa Jumamosi ya  mwisho wa mwezi  Machi  kila mwaka yenye kampeni isemayo '60 Earth Hour'.


Amesema kuwa Mto Msimbazi kwa sasa unategemea maji ya mvua tu kwa kipindi cha msimu wa mvua na inapofika wakati wa kiangazi maji yanayotiririka ni maji taka kutoka katika makazi ya watu.

Yusuf ameeleza kuwa uhifadhi wa miti   ni suala mtambuka kila mtu, anajukumu na anapaswa kujifunza huku akisema   katika suala hilo Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF),limewashirikisha wanafunzi wa shule  za sekondari na msingi walipo karibu na mto Msimbazi kwa lengo la kushiriki kupanda miti hiyo pamoja na kuwapatia elimu na kuwajengea uelewa wa kutunza mazingira.

"Tupo hapa ndani ya msitu wa Pugu kazimzumbwi pembezoni mwa mto Msimbazi, ndani ya bonde la mto Msimbazi tukipanda miti katika kuelemisha jamii  siku ambayo WWF wanaiadhimisha dunia nzima ambayo inatwa Earth Hour, tukio ambalo wamelichagua ni kupanda miti katika utekelezaji wa mradi ambao unaendelea ya kulighuisha bonde hili ili kuongeza kiwango cha maji kutiririka ndani ya mto na kuwezesha maji haya kuwa yenye ubora kwa matumizi ya binadamu na matumizi mengine ya kiafya," amesema.


Amesema kuwa katika mto,bonde la msimbazi kuna miradi miwili inayoendelea ambayo ni mradi wa Mkondo wa chini 'Lower streem' na Mkondo wa juu 'Upper streem'.

Amefafanua kuwa mradi wa Mkondo wa juu unatekelezwa na WWF kupitia Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu ni mradi ambao unaangalia ni kwa namna gani ya kuweza kulitunza bonde hilo na kupandwa miti lengo likiwa ni kuongeza mtiririko wa maji katika mto huo na kusababisha maji hayo kuwa bora na ya kiwango.

"Mimea imebeba maji asilimia 80 ili maji yanayotiririka yawe na nafasi ni lazima kupanda miti na kuihifadhi.Mradi huo utakapokamilika kupanda miti kiwango cha maji ya kutiririka yataongezeka na kuwa na ubora wa kiwango cha hali ya juu katika matumizi ya binadamu," ameeleza.

Yusuf ameongeza kuwa  katika tabaka la dunia la juu maji yamegawanyika katika pande kuu mbili ambayo ni maji ya kijani (Green water) na maji ya bluu (blue water),huku akifafanua kuwa maji ya bluu ni yale yanayotiririka na ya kijani hayaonekani kwa sababu yamebebwa ndani ya mimea.


Naye Meneja Mawasiliano wa WWF, nchini Tanzania Joan Itanisa amesema uhifadhi wa mazingira ni suala la mtambuka ambalo linapita kila mahali.

Ameongeza kuwa WWF wameona waitumie siku hiyo kuhamasisha watu waweze kujitokeza popote walipo wanavyoweza ili kushiriki katika uhifadhi wa mazingira na kwamba wanahamasisha watu walahu watumie dakika 60 kwa kufanya jambo la uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kufanya usafi, kupanda miti  na kutoa elimu.

"Leo tumeadhimisha  wasaa wa mazingira 'Earth Hour' hii ni siku ambayo tunaiadhimisha kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi Machi ikilenga kuhamasisha wanajamii wa kawaida kuweza kushiriki katika utunzaji wa mazingira,sio taasisi,sio serikali sio mashirika," amesema Joan.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Baiskeli Mkoa wa Dar es salaam Hussein Ally amesema kuwa wamehamasika kuungana na WWF kupanda miti ambapo wameendesha baiskeli zao kutoka Tazara daraja la Mfugale hadi Pugu kilometa 18 lengo likiwa ni kuwahamasisha Watanzania katika suala la uhifadhi wa mazingira.

"Watanzania wengi tunakuwa nyuma katika masuala ya utunzaji wa mazingira na hatujui hasa dhana halisi ya mazingira, hawa WWF kwa kushirikiana na chama cha Waendesha baiskeli na wadau wengine tumehamasika kuja hapa kuhakikisha bonde la mto huu linabaki kuwa na uoto wa asili,"ameeleza.


Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA