TANZANIA KUFANYA MAONESHO YA SABA YA UTALII, (SWAHILI INTERNATIONAL TOURISM EXPO-S!TE), OKTOBA


Na Beatrice Sanga

WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii nchini (TTB) imezindua onyesho la Saba la Kimataifa la utalii maarufu kama Swahili International Tourism Expo-SITE.

Hayo yamesemwa Aprili 25, 2023 na Mkurugenzi wa Bodi ya utalii Tanzania (TTB), Damas Mfugale wakati akizundua rasmi onyesho hilo ambalo linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Mlimani City Jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 06 hadi 08 Oktoba mwaka huu.

Mfugale amesema, onesho hili linatarajiwa kuhudhuriwa na waoneshaji zaidi ya 200 na wanunuzi wa kimataifa takribani 150 kutoka katika masoko ya utalii ya msingi na yale yanayochipukia hususani nchi za Marekani, Uingereza, Italia, Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi, Canada, Australia, Hispania, Arika Kusini, Nchi za Ghuba, India, China, Uturuki, Brazili Czech Poland na Urusi ambao watapata fursa ya kununua na kuuza bidhaa mbalimbali za utalii.

“Onesho hili la SITE 2023 litahusisha utangazaji wa bidhaa mbalimbali za utalii, Jukwaa la uwekezaji, Semina kuhusu masuala ya utalii na masoko, na mikutano ya wafanyabiashara za utalii,” amefafanua Mfugale.

Aidha Mfugale amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo ambayo itakuza Sekta ya Utalii hapa nchini ikiwa ni katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii kupitia Filamu ya The Royal Tour aliyoifanya mapema mwaka 2022 kwaajili ya kukuza utalii na kuongeza Pato la Taifa sambamba na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 pamoja na mkakati wa kutangaza utalii Kimataifa wa mwaka 2020-2025.

“Naomba kutoa rai kwa wadau wa utalii waliopo ndani na nje ya nchi hususan mawakala wa biasara za utalii, watoa huduma za malazi, mawakala wa safari na waongoza watalii kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zitakazotokana na onesho la S!TE, fursa hizo ni pamoja na kutangaza biashara zao kutengeneza mtandao wa biashara na kutoa huduma mbalimbali wakati wa onesho la S!TE.” 

Aidha ameeleza kuwa kutakuwa na siku sita za ziara za mafunzo (Fam trips) zitakazohusisha kutembelea vivutio vya utalii hapa nchini ikiwemo hifadhi za Taifa za Kilimanjaro na Mkomazi, Hifadhi ya Ruaha na vivutio vingine vilivyopo mkoani Iringa, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na eneo la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Saanane, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, na magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara na visiwa vya Zanzibar.

“Nawaomba ndugu zangu watanzania pamoja na waandishi wa habari na vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika mambo ya kuhamasisha na kutangaza onesho hili, pili kupigia kura vivutio vyetu vilivyoingia kwenye mashindano ya vivutio vinavyoongoza na Taasisi bora duniani (World Travel awards 2023) ambavyo ni hifadhi ya taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, bonde la Ngorongoro na Taasisi za bodi ya utalii Tanzania uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere, Mamlaka ya bandari Tanzania na visiwa vya Zanzibar.” Amefafanua Mfugale.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bank ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema kuwa hii ni fursa kwa wafanyabiashara kukuza biashara zao na kujitangaza zaidi kupitia onesho hilo.

“Kwa kuwa na S!TE hii TTB na wadau wengine watatangaza maeneo mazuri ya Tanzania, lakini wakitangaza habari zaidi za kitanzania na watu kutoka dunia wataijua Tanzania na tutapata watalii wengi, lakini siyo watalii tu kutakuwepo na fursa za uwekezaji na wapo wengi wangependa kuja kuwekeza hapa aidha kwenye uchumi wa bluu, au kwenye hoteli na sekta mbalimbali.”

Onesho la SITE lilianza mwaka 2014 likiwa na lengo la kuvutia watalii wengi kupitia wanunuzi wa kimataifa na waandishi wa makala za safari kutoka sehemu mbalimbali duniani, lakini pia onesho hili huhudhuriwa na wafanyabiashara za utalii wa kimataifa kutoka ndani na nje ya Tanzania ambao hupata fursa ya kuonesha bidhaa mbalimbali za utalii, na tangu kuanzishwa kwake onesho hilo limekuwa na mafanikio ikiwemo ongezeko la waoneshaji na wanunuzi wa kimataifa ambapo kati ya mwaka 2014 na 2019 na baadae 2022 waoneshaji waliongezeka kutoka 40 hadi 170 na wanunuzi wa kimataifa waliongezeka kutoka 24 hadi 333.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU