Na Asha Mwakyonde,Dodoma
MHITIMU wa Mafunzo ya Useremala kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA ),Chuo cha Ufundi Stadi VETA Kihonda Morogoro Rashid Mahonge amewashauri vijana kujiunga na VETA ili wakajifunze fani mbalimbali ambazo zitawasaidia katika kuzalisha bidhaa ambazo zitawainua kiuchumi wao na Taifa Kwa ujumla.
Akizungumza jijini Dodoma Aprili 25,2023 katika banda la Mamlaka hiyo kwenye maonesho ya wiki ya Ubunifu Kitaifa (IWTZ), yenye kaulimbiu isemayo "Ubunifu Kwa Uchumi shindani,"ambayo yanaendela katika viwanja vya Jamuhuri
Mahonge amesema kila wilaya kuna Vyuo vya VETA ambapo ni fursa kwa vijana kwenda kujifunza na kujipatia ujuzi wa fani wazipendazo.
Mahonge ameongeza kuwa baada ya kuhitimu VETA ameanzisha karakana, kiwanda chake cha kutengeneza bidhaa mbalimbali za mbao zikiwamo bakuli za kuwekea sukari, vishikia funguo, meza,stuli, saa za mbao pamoja na viti.
"Wiki hii ya ubunifu nimekuja na bidhaa hizi za mbao kama hivi viti na meza havichukui nafasi kwa kuwa baada ya matumizi unaweza kuvikunja na kuweka pembeni," amesema Mahonge.
Ameongeza kuwa hiyo ni faida ya mafunzo aliyoyapata kutoka VETA huku akisema lengo la kutengeneza bidhaa hizo ni kukabiliana na hali ya kiuchumi ikiwamo kujikimu na familia yake.
"Hiki ni chanzo cha ajira tumeshirikiana na wenzangu kutoa bidhaa iliyobora nimeajiri watu ambao nao wanajipatia kipato," amesema mhitimu huyo.
Amefafanua kuwa VETA imewawezesha kupata elimu ambapo alisoma hadi ngazi ya tatu hali iliyomsaifia kuanzisha kiwanda mkoani Tanga ambacho kimeajiri wafanyakazi wawili.
Akizungumzia matumizi ya mbao amesema kuwa serikali imepiga marufu uchomaji wa mkaa ambao chanzo chake ni miti hivyo bidhaa zake anatumika mabaki ya mbao zilitotumika kutengeneza milango na bidhaa nyingine.
Akizungumzia matarajio yake Mahonge amesema ni kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya wateja wake
0 Comments