Chifu Mtemi Mazengo wa ii akionesha eneo ambalo Tembo alizama wakati anakunywa maji.
Kisima cha maji kinachutumiwa na Chuo cha Mtakatifu John maarufu kama St.John kilichochimwa katika mkono wa maji alipozama tembo.
Na Asha Mwakyonde,Dodoma
KABLA ya mwaka 1912 Dodoma ilikuwa inafahamika kama Idodomia baada ya Tembo kuzama akiwa anakunywa maji katika eneo la Kikuyu, Kata ya Kikuyu Mtakatifu John maarufu kama St. John's.
Miaka mingi iliyopita mji wa Dodoma ulikuwa ukifahamika kama Calangu (Chalangu) mji huo haukuwa na wenyeji bali ulikuwa na wahamiaji toka maeneo mbalimbali ambao ni wamanghala, wabambali, wayenzele na wanghulimba.
Wahamiaji hao walikuwa wakitofautiana kwa tabia na tamaduni zao, wamanghala na wabambali waliishi msituni na walikuwa wawindaji wakila nyama na asali.
Akizungumzia historia ya jina la Dodoma Chifu Mkuu wa Kanda ya Kati Dodoma
Mtemi Mazengo wa ii amesema kuwa mwaka 1912 alifika Mjerumani wa kwanza Mjini Dodoma, Dk.Spreling (Spelenje), akiwa lengo la kujua historia ya Idodomia ambapo sasa inaitwa Jiji la Dodoma.
Chifu huyo amesema kuwa baada ya Tembo kuzama katika eneo hilo wakati anaingia kutafuta maji ili anywe ndipo alipodidimia na kuzama ambapo wenyeji wa mji huo wakasema Tembo yadodomela wakimaanisha amedidimia.
Chifu Mazengo wa ii amefafanua kuwa mzungu huyo aliposhindwa kutamka Idodomia ndipo aliposema Ooh! Dodoma ndipo likazaliwa jina la Dodoma ambalo linatumika hadi leo.
"Hapa ndipo asili ya Dodoma ilipoanzia
Katika eneo hili kulikuwa na neema ya maji wakati wa kiangazi na masika miaka ya 1909 ilikuwa ni njia ya kupita Tembo,"amesema Chifu Mazengo wa ii.
Amesema kutokana na eneo hilo kuachwa, kutelekezwa na serikali watu walivamia na kuanza kujenga ambapo wao kama machifu wenye kujua historia walizuia ujenzi huo.
"Nawashukuru waandishi wa habari mnaofuatilia vitu kama hivi,tunatamani kuona wahusika wakija kulitengeneza eneo hili ili liwe kivutio kwa vizazi vijavyo hapa ndio asili ya Dodoma ilipotokea," ameeleza.
Aidha Chifu Mazengo wa ii amewaomba wanaohusika na masuala haya waje wajenge ili eneo hili litambulike kama kivutio ambapo vizazi zijavyo watavikuta.
JITIHADA ZA MACHIFU
Akizungumzia jitihada wanazozifanya machifu wa Dodoma za kuhakikisha eneo hilo halivamiwi tena wanalitembelea mara kwa mara hata aliyevamia kujenga walisimama kidete ili ujenzi usiendelee na kwamba wanasubiri aliyevamia wamalizane na Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru kwa kuwa suala hilo lipo mezani kwake.
Chifu Mazengo ameongeza kuwa suala hilo likiisha wanatarajiwa kukabidhiwa eneo hilo ambapo wataendelea kusisimamia na kubaki eneo la wazi na kuheshimiwa kama ilivyo sasa.
Chifu Mazengo ameeleza kuwa eneo hilo muda mwingine wanalitumia kufanya Mila za kabla la wagogo huku akiomba litunze kwa kujenga vivutio ambavyo watu na wageni wanaofika Jijini Dodoma kwenda kutembelea.
"Katika eneo hilo alipozama Tembo baada ya kuanzishwa shule ya Mezingo sekondari ndipo kukachibwa kisima cha maji lengo ni kuwasaidia wanafunzi
na pia eneo hili ndio lenye maji mengi, huu ni mkondo wa maji umepita hapa," amesema Chifu Mazengo wa ii.
Kutokana na mazingira yaliyo sasa watu kujenga makazi Chifu huyo amesema kuwa mkondo wa maji umepotea na kwa hata mtu akiambiwa kulikuwa na mkondo huo hawezi kuamini.
"Miundombinu iliyokuwepo zamani imeshasharibiwa na makazi ya watu, mmeiona hii mikuyu inapenda kuota kwenye maji mengi ndio maana eneo hili likaitwa Kikuyu ilikuwa mingi," ameeleza.
Amefafanua kuwa maji yaliyokuwa yakitririka wanyama na binadamu walikuwa wanatumia wote na kwamba hawakuweza kupata maradhi ya aina yoyote kwa wakati ule.
SHUKURANI KWA RAIS SAMIA
Chifu Mazengo amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia vivutio visipotee huku akitoa wito kwa Shirika la Hifadhi za TAIFA Tanzania (TANAPA), ambao ndio wahusika wakuu waliangalie eneo hilo kwa jicho la pili nakuweza kuliboresha ili liwe kumbukumbu kwa Mkoa wa Dodoma.
Emmanuel Juma ni mwenyeji wa Musoma wilaya Tarime ambaye yupo mkoani hapa akijishughulisha na usafirishaji abiria (Boda boda),kutoka kituo cha Matakatifu John kwenda sehemu mbalimbali amesema kuwa katika kituo chao hicho ndio asili ya Dodoma alipozama tembo.
"Serikali imeshindwa kutambua mchango wa eneo hili hadi sasa hakuna kiashiria chochote kinachoonesha jina au asili ya Dodoma ambapo ilianzia hapa, hata kwenye vyombo vya habari tukiangalia tunaona majengo makubwa yakionesha ndio Dodoma bila kujua asili yake ilianzia wapi," amesema.
Aidha ameiomba serikali kuwatengenezea makumbusho ya asili katika eneo hilo huku akisema, sehemu ni kubwa ingeweza kuleta hata mapato kwa Kata ya Kikuyu na Jiji kwa ujumla.
Juma ameongeza kuwa eneo hilo likihifadhiwa watu mbalimbali watafanya utalii wa ndani na hata watakao toka nje ya nchi wataongeza Pato la Taifa kwa kufika kuangalia vivutio na kupata historia ya Mkoa wa Dodoma.
Amebainisha kuwa eneo hilo kwa sasa ni chafu halijalimwa na halioneshi historia ya Dodoma kama imeanzia hapo na kwamba mtu hawezi kuelewa kama kulikuwa na mkondo wa maji na tembo aliwahi kuzama.
0 Comments