WAZIRI UMMY: WAGONJWA WENYE SHINIKIZO LA JUU LA DAMU WAMEONGEZEKA MARA MBILI


Waziri wa Afya Ummy Mwalimu  akizungumza na waandishi wa habari hawapo (pichani), wakati akitoa tamko kuhusu Shinikizo la Juu la Damu.


Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akipimwa Shinikizo la Juu la Damu.

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

WAGONJWA wenye Shinikizo la juu la damu wameonekana kuongezeka takribani mara mbili zaidi kwa kipindi cha miaka mitano (Health Statistical Bulletin 2022 kutoka wagonjwa 688,901 mwaka 2017 hadi kufikia 1,345,847 mwaka 2021 sawa na asilimia 95.4.

Takwimu kutoka kwenye mfumo wa ukusanyaji taarifa za afya (DHID2),nchini Tanzania zinaonesha jumla ya wagonjwa 2,535,281 walitibiwa magonjwa yasiyoambukizwa kwenye vituo vya afya  mwaka 2017, wagonjwa hao wameongezeka  hadi kufikia 3,440708 mwaka 2021.

Akizungumza jijini Dodoma leo Mei 17,2023 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akitoa tamko kwenye maadhimisho ya siku ya Shinikizo la juu la damu duniani yenye kaulimbiu isemayo "Pima Shinikizo la Damu Kwa  Usahihi, Idhibiti, Ishi kwa Muda Mrefu" amesema ongezeko hilo la wagonjwa wako 905,427 kwa kipindi hicho cha miaka mitano sawa na ongezeko la asilimia 94.

Waziri Ummy  ameeleza kuwa tangu Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ilipoanzishwa Septemba 2015 hadi Aprili 2023 kati ya  wagonjwa 619,102 waliowatibia asilimia 66 ya wagonjwa walikuwa na tatizo la Shinikizo la juu la damu ikiwa na maana kila wagonjwa 10 wanaoonwa katika taasisi hiyo 6 wana ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa uchunguzi uliofanywa katika jamii kwenye mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara,Lindi Iringa na Dar es salaam takwimu zinaonesha watu  watatu hadi wanne  kati ya 10  wana ugonjwa huo.

Waziri huyo amesema ugonjwa huu ndio sababu kubwa (vihatarishi) ya kihausi (Stroke), shambulio la moyo (Heart attack), moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure), kutuna kwa Kuta za mishipa ya damu, moyo,uharibifu kwenye chujio za figo, ganzi miguuni  na mikononi, upofu na kupunguza nguvu za kiume kwa wanaume.

"Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dk. Samia inaendelea na utekelezaji  wa sera ya afya ya mwaka 2007 ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu kwa umahiri zaidi, amesema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amewaomba wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kuepuka ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu.


Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Profesa Paschal Ruggajo amesema kuwa  Watanzania ambao wamefikisha umri wa zaidi  ya miaka 30 inakadriwa Watanzania milioni 6 wanashinikizo la juu la damu kati yao ni milioni 1.4 tu ndio walioweza kufikiwa, kupima na kujitambua kuwa wanaugonjwa huo.

Amesema wananchi wenye umri wa zaidi ya miaka 30 milioni 4.6 hawajui au wanaishi na kwamba hawajawahi kupima  na kutambua kama wana ugonjwa huo.

"Tunamshukuru Waziri Ummy kwa kulipa uzito siku ya leo kwa kutoa tamko na tumeyapokea maelekezo yake aliyoyatoa tunaendelea kuyatekeleza katika muktadha mzima wa kuboresha afya za Watanzania," ameeleza.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI