DAWA ZA KUPUNGUZA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU ZASHUSHWA HADI KUFIKIA NGAZI YA ZAHANATI


Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imesema kuwa mwaka huu imeamua kupeleka dawa za kupunguza ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu (Hypertention),kwenye afya ya msingi.

Akizungumza  hivi karibuni jijini Dodoma mara baada ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kutoa tamko katika maadhimisho ya siku ya Shinikizo la juu la damu duniani yenye kaulimbiu isemayo "Pima Shinikizo la Damu kwa Usahihi, Idhibiti, Ishi kwa Muda Mrefu", Mkurugenzi wa Huduma za Tiba  kutoka Wizara ya Afya Profesa Paschal Ruggajo amesema kuwa dawa tatu ambazo zimeshushwa kutoka Hospitali ngazi ya Wilaya, Halmashauri kwenda ngazi ya kituo cha afya ni Losartan,Amlodipine na Hydralazine.

Prof. Ruggajo ameeleza kuwa dawa hizo 
 zimeshushwa kutoka hospitali ya Wilaya zinakwenda katika hospitatli ngazi ya kituo cha afya hivyo hivyo,kuna dawa mbili ambazo zimetoka ngazi ya kituo cha afya kwenda ngazi ya zahanati ambazo ni Nifedipine na Furosemide.

"Serikali imechukua hatua za makusudi na kuweza kupunguza uwezekano wa kupata madhara ya kukaa muda mrefu mgonjwa anapopewa Rufaa kutoka kwenye ngazi ya msingi kwenda ngazi za juu," ameeleza.

Prof. Ruggajo ameongeza kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika vifaa tiba, miundombinu na watumishi pamoja na kuendelea kupeleka ugunduzi mapema kwenye matibabu ya ugonjwa huo katika afya ya msingi kwenye zahanati na vituo vya afya.

Amesema kwa kiasi kikubwa serikali imejitahidi kuwekeza kwenye Hospitali za  mikoa, Kanda, Rufaa na Hospitali maalumu huku akisema wananchi wengi bado wanatafuta huduma katika afya ya msingi.

Prof. Ruggajo amesema kwa kushirikiana na wadau wamesambaza vifaa tiba, wamefanya mafunzo na kwamba serikali baada ya kugundua wananchi wengi wanatibiwa kijijini na matibabu ya Shinikizo la juu la damu yanatakiwa yaanzie kule ili kuepuka matatizo.

Amewataka wananchi kuwa na programu maalumu za kujipangia 
 maisha ambayo ni ya kuongeza ubora  na kupunguza matatizo katika maisha hayo huku akiwataka Kwenye ngazi ya familia kusisitizana, shuleni kupima na kufundisha kwenye mitaala kuhusiana na Shinikizo la juu la damu.

Amesema pia kazini, wafanyakazi waweke siku za kuhakikisha wanatangaza michezo, kukumbushana lishe ambayo inastahili ikiwa ni pamoja na kuweka misingi ya kujiliwaza na kupumzika kidogo ili kupunguza msongo wa mawazo ambao unachangia kuongeza Shinikizo la juu la damu.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI