Na WAF- Bungeni, Dodoma.
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameweka wazi kuwa, Serikali imepanga kuchukua hatua kali kwa wote wataobainika kwenye upotevu wa dawa ili iwe funzo wengine wenye nia ovu ambayo inawanyima wananchi haki yao ya msingi ya kupata huduma hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma nchini.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Mei 23, 2023 wakati akijibu swali la Mhe. Luhaga Joelson Mpina katika Mkutano wa kumi na moja kikao cha 31, Bungeni Jijini Dodoma.
Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya iliona dalili za upotevu wa Bilioni 83 hivyo kushirikiana na TAKUKURU ili kuhakikisha wote wataobainika kuwepo katika upotevu huo wa dawa wanachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia hiyo.
Amesema, Serikali imefanya mikakati mbalimbali katika kutatua tatizo la wizi na ubadhilifu wa dawa na vifaa tiba ikiwemo kufanya suala la upotevu wa dawa na vifaa tiba kama agenda katika vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya.
Ameendelea kusema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa bidhaa za Afya ikiwemo kufunga mifumo ya kielectroniki pamoja na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa bidhaa hizo.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Wizara kwa kushirikiana na OR TAMISEMI imeendelea kuimarisha kamati za usimamizi za vituo kwa kuzijengea uwezo kuhusu majukumu yao katika usimamizi wa bidhaa za Afya.
Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amesema, Wizara imeendelea kutoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wabunge kushiriki katika upokeaji wa bidhaa hizo na taarifa zote wapewe ili kujenga uwazi zaidi juu ya bidhaa hizo za afya.
Aidha, Dkt. Mollel amesema suala la kupambana dhidi wizi na ubadhilifu wa bidhaa za Afya siyo la Serikali pekee bali ni suala la kushirikiana pande zote, hasa wawakilishi wa wananchi.
0 Comments