Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum,Dk. Dorothy Gwajima amesema kuwa mmomonyoko wa maadili kwa wananchi ni tatizo linaloweza kusababisha kutokufikia malengo wanayohitaji yakiwamo huduma bora za afya, miundombinu na nyinginezo.
Akizungumza jijini Dodoma Mei 11,2023 wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Waziri Dk. Gwajima ameeleza kuwa mstakabali wa Taifa lolote duniani linategemea michango ya taasisi na wadau ili kuyafikia malengo.
Dk.Gwajima ameongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho wanachopambana kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto mara nyingi mashauri ya ukatili yanapojitokeza huwa yanasimamiwa na afisa wa jamii chini ya sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
"Wizara hii ina kada mbili ambazo ni taaluma ya Maendeleo ya jamii na taaluma ya Ustawi wa jamii hivyo manusura anakapopata tatizo ataripoti katika kituo cha polisi ambapo huduma zimeboreshwa kwa kutengeneza madawati ya kijinsia na huduma kwa watoto ndipo manusura atakapokutana na afisa wa polisi na afisa Ustawi wa jamii na afisa wa sheria," amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii Fatma Toufiq amesema kati ya Wizara inayotakiwa kuangalia kwa jicho la tofauti ni wizara ya maendeleo ya jamii ambayo inajukumu kubwa la kuhakikisha jamii inakuwa salama katika masuala ya ukatili.
"Natambua wizara hii ni mtambuka na natamani iende mbalii zaidi
katika bajeti inayokuja Wizara hii iweze kuangaliwa kwa jicho la tofauti na kupewa kipaumbele," ameeleza Mwenyekiti huyo.
Akitoa mada kwa Kamati hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum,Patrick Golwike amesema baadhi ya vigezo vya kupima maendeleo ya jamii ni ongezeko la huduma pamoja na ongezeko la mapato.
"Tafsiri ya maendeleo ya jamii inategemea aina na mazingira mfano tamaduni,hatua ya maendeleo iliyofikiwa na namna jamii ya mahali fulanai inavyotafsiriwa," amesema.
Mkurugenzi Msaidizi Vyuo vya Maendeleo ya jamii Neema Ndoboka amesema wizara hiyo ina Vyuo nane huku akifafanua kuwa Vyuo sita vinatoa kozi ya maendeleo ya jamii na viwili ambavyo ni Vyuo vya Mabaghai kilichopo Lushoto Tanga na Misungwi Mwanza ambavyo vinatoa kozi ya Uhandisi wa ujenzi wa maendeleo ya jamii.
Ameongeza kuwa wahitimu wa Vyuo hivyo wanaajiriwa katika mamlaka za serikali za Mitaa, taasisi zinazofanya kazi za maendeleo ya jamii.
0 Comments