TRA YAWAFUATA WAFANYABIASHARA KUWAPATIA ELIMU YA EFDs


Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

WAFANYABIASHARA ambao bado hawajaanza kutumia Mashine za Kielektroniki za EFDs wametakiwa kujitathimini wao wenyewe na kuwaita wataalam wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),kuwafanyia tathimini kujua mwenendo wa mapato yao na endapo watatimiza vigezo vya kutumia mashine hizo waanze kuzitumia.

Pia TRA imeshauriwa kununua mashine hizo nyingi na kuzigawa kwa wafanyabiashara bure lengo ni kuwafikia wafanyabiashara hao kwa asilimia 20 ya 'Tax base' na baadae mamlaka hiyo kuchukua kodi kutokana na mauzo.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma Mei 13,2023 na Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri wakati TRA ikiendesha kampeni ya "Tuwajibike" yenye lengo la kutoa elimu kuhusu matumizi ya mashine hizo katika eneo la Meliwa ameeleza kuwa matarajio ya serikali ni kuona ukusanyaji wa mapato unaimarika ili kuiwezesha kufanya kazi zake za mipango ya maendeleo ambayo yanatafsiriwa kwenye bajeti ya serikali kuu.

Amesema lengo la TRA la ukusanyaji mapato kwa mwaka mzima ni trillioni 23 sawa na wastani wa trilioni 1.9 hadi 2 kwa mwezi na kwamba kuna wakati walifika 2.7 kwa kukusanya kodi.

"Wote tunawajibu wa kuisaidia serikali kwa kumsaidia Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye anafanyakazi nyingi na maeneo mengi nchi nzima lakini hapa Dodoma maendeleo ni mengi zaidi, sisi kodi inavyokusanywa tunaiona moja kwa moja kupitia miradi mikubwa iliyopo hapa kwetu," amesema Shekimweri.

Aidha amewashauri wajasiriamali na wananchi  wanaponunua bidhaa zao kudai risiti za EFDs ili kutoa mchango kwa serikali kupitia mananuzi yao na kwamba wasipodai risiti hizo mfanyabishara ataidhulumu serikali.


Akizungumzia kampeni ya Tuwajibike Meneja Msaidizi wa TRA Mkoa wa Dodoma Ramadhani Sengo amesema kuwa kampeni hiyo inalengo la kuhamasisha wauzaji kutoa risiti kwa kila mauzo wanayoyafanya na wanunuzi kudai risiti halali kwa manunuzi yote wanayoyafanya.

"Tumekuwa na zoezi la kuwatembelea wafanyabiashara wetu siku nzima ya leo kwa ajili ya kuwaelimisha  juu ya wajibu wao wa kutoa risiti na wateja wetu  kudai risiti  halali inaoyoonesha kiwango cha fedha walichokitoa pindi wanapofanya  manunuzi ya bidhaa mbalimbali," amesema Sengo.

Amefafanua kuwa lengo jingine la kampeni hiyo ni kuendesha ukaguzi wa wafanyabiashara ambao hawatumii mashine hizo kwa kuwa kutokuzitumia ni kosa kisheria huku akisema atakayekutwa hatumii mashine za EFDs hatua kali dhidi yake zitachukuliwa.

Awali Afisa Msimamizi Kodi Mwandamizi Kitenge cha Huduma  Elimu ya mlipata kodi kutoka TRA Dodoma Philip Eliamini  ameeleza kuwa mfanyabiashara anapofikisha mauzo ya milioni 11 kwa mwaka anapaswa kuanza kutumia mashine za EFDs.

"Na kwa wale ambao tunawakuta tayari wameshifikisha kiwango hiki tunawapa barua na muda wa kuwataka waanze kuzitumia mashine hizi, pia tutoe rai kwa wafanyabiashara wenyewe ambao wamejitathimini na kuona wamefikisha mauzo ya milioni 11 kwa mwaka wafike ofisi za TRA waweze kusajili," amesema.


Mmoja wa wafanyabiasha wa duka la huduma za watoto katika eneo hilo Restuta Remedius akizungumzia matumizi ya mashine hizo amesema kuwa ana muda wa mwezi mmoja ambapo biashara yake ina muda wa zaidi ya mwaka mmoja.

Amesema kuwa faida ya matumizi ya mashine hizo ni kumletea uaminifu kwa bosi wake kwa kuwa kila anachokiuza kinaonekana kwenye risiti pamoja na kumrahisishia mahesabu yake ya mauzo.

Restuta amewataka wafanyabiashara wenzake kutumia mashine hizo kwa maendeleo ya nchi wasiwe wahujumu uchimi.


Naye mkazi wa Dodoma Rajabu Kibwana akitoa maoni yake juu ya matumizi ya mashine hizo amesema kuwa miradi mingi ya maendeleo inawezeshwa na fedha za kodi.

Amewashauri wafanyabiashara kutoa risiti na wateja kudai risiti hizo zenye uhalali na fedha iliyotolewa lengo likiwa ni kuijenga nchi kwa kuwa inajengwa na wananchi wenyewe.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI