BRELA YAWAHIMIZA WAJASIRIAMALI KULINDA BIASHARA ZAO KISHERIA


Tanga 

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imewahimiza wajasiriamali mkoani Tanga kulinda biashara zao kisheria kwa kusajili Alama za Biashara na Huduma wanazotoa, ili waweze kutambulika katika masoko na kuzilinda kisheria. 

Ushauri huo umetolewa na Afisa Usajili wa BRELA, Bi. Julieth Kiwelu,  kwenye mafunzo ya wajasiriamali yaliyofanyika  Juni 5, 2023, sambamba na Maonesho ya Biashara, Utalii na Uwekezaji katika uwanja wa Mwahako, jijini Tanga.

Bi. Kiwelu ameeleza kuwa mjasiriamali anaposajili  Alama ya Biashara na Huduma inamsaidia bidhaa yake kutambulika katika masoko na inamlinda mjasiriamali kumiliki alama ya bidhaa kisheria, hivyo ni kosa kisheria kwa mfanyabiashara mwingine kutumia jina au alama inayofanana  na bidhaa yake. 

 Amewasisitizia wajasiriamali kusajili Alama za Biashara na Huduma ili bidhaa zao ziweze kutofautishwa na bidhaa nyingine zinazozalishwa, zenye ufanano na usajili huo utasaidia kwenye ushindani wa kimasoko. 

Pia, katika mafunzo hayo amewaeleza washiriki umuhimu wa kusajili Majina ya Biashara ili kutambulika kisheria hatua itakayowawezesha   kupata huduma nyingine kutoka taasisi  mbalimballi zikiwemo za fedha.

Katika mafunzo hayo  wajasiriamali hao pia wamepewa elimu juu ya utaratibu wa kupata  Hataza, Leseni za Biashara kundi "A" na Leseni ya Kiwanda na usajili wa Kiwanda Kidogo.

BRELA inashiriki kwenye Maonesho ya Biashara, Utalii na Uwekezaji ikitoa huduma za sajili, utoaji wa leseni, elimu na ushauri kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA